Search This Blog

Monday, March 1, 2021

Wanne wafariki kwa ajali wakitokea kwenye mapumziko


Na Amiri Kilagalila,Njombe.

Watu wanne akiwemo mkuu wa chuo cha uuguzi Lugarawa Steven Mtega (39) wamefariki dunia kwa kuzama kwenye mto Lupali wakiwa kwenye gari waliyokua wakisafiria kata lugarawa wilayani Ludewa mkoani Njombe.

Akizungumza kwa njia ya simu jana mganga mkuu  wa wilaya ya Ludewa dkt Stanley Mlay,alisema tukio hilo limetokea febuari 27 majira ya usiku marehemu hao walikua kwenye gari aina ya harrier ambapo walikua Lugarawa kwenye mambo yao ya mapumziko.

"Walipata ajali kwenye mto lupali huu mto sasa hivi una maji mengi kwa sababu ya mvua zinavyonyesha walikua watu wanne kwenye mambo yao ya mapumziko Lugarawa na dereva alikua huyo mkuu wa chuo wakasema wabadilishe maeneo waende Mundindi sasa walivyofika maeneo hayo ndo wanaingia mtoni" alisema Mlay.

Mlay aliwataja marehemu wengine kuwa Marko Mpete,fundi umeme wa Lugarawa

Merk Mwalongo(35)mjasiriamali

Rukia Mfaume(28) alikuwa mhasibu wa mradi wa umeme wa Akra Lugarawa

Hata hivyo alisema miili ya marehemu hao iko chumba cha kuhifadhia maiti(Mochwari)Hospital ya Lugarawa ikisubiri taratibu za mazishi kukamilishwa.

Naye diwani wa kata ya Lugarawa Erasto Mhagama,akizungumza kutokea kwa tukio hilo alisema tukio hilo limetokea mpakani kwa kijiji cha shaurimoyo na kijiji cha amani.



Marekani iko tayari kwa mazungumzo na Iran juu ya makubaliano ya nyuklia


Utawala wa Rais wa Marekani Joe Biden umesema unaridhia kufanya mazungumzo na Iran juu ya makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015 licha ya Iran kukataa mualiko wa Umoja wa Ulaya kujiunga na mkutano na Marekani na washirika wengine kwenye makubaliano hayo.

 Afisa mmoja mwandamizi amesema Marekani imehuzunishwa na hatua ya Iran kukataa mualiko huo. Afisa huyo mwandamizi amesema Marekani itashauriana na washirika wengine ambao ni Uingereza, China, Ufaransa, Ujerumani, Urusi na Umoja wa Ulaya juu ya hatua zaidi za kufanya. 

Afisa huyo haruhusiwi kuzungumia juu ya suala hilo na alifanya hivyo kwa sharti la kutotambulishwa. Mapema Jumapili, Iran ilikataa ofa ya mazungumzo ikisema kuwa sio wakati sahihi kwa mkutano huo, mkutano ambao Marekani ingeshiriki kama muangalizi. 

Iran imekuwa ikisisitiza kuwa Marekani inafaa kuondoa au kulegeza vikwazo ilivyowekewa na utawala uliopita wa Donald Trump chini ya kampeni yake ya kuiwekea mbinyo Iran.



Kikosi cha wachezaji wa KMC kuwafuata Polisi Tanzania kesho


Kikosi cha KMC FC  kesho kitaondoka jijini Dar es Salaam kuelekea Jijini Arusha katika mchezo wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara dhidi ya Polisi Tanzania utakaopigwa Machi Nne katika uwanja wa Sheikhe Amri Abeid.

Katika msafara huo wa wana Kino Boys, utakuwa na wachezaji 24, Benchi la ufundi pamoja na Viongozi  ambapo KMC FC  inakwenda Jijini Arusha kusaka alama tatu muhimu ikiwa ugenini.

Aidha KMC FC katika mchezo huo inakwenda ikiwa imejipanga kupata ushindi ambapo katika michezo ya nyumbani imefanya vizuri kwa michezo miwili mfululizo ya Ligi kuu sambamba na mchezo mmoja wa michuano ya Kombe la Shirikisho kwa ushindi wa magoli matano kwa mawili dhidi ya Kurugenzi kutoka Mkoani Simiyu.

Kino Boys inahitaji ushindi katika mchezo huo kwani katika duru ya kwanza ilipoteza mchezo dhidi ya wapinzani wake Polisi Tanzania kwa kuifunga goli moja kwa sifuri  katika uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam

“Kesho tunakwenda kuwafuata Polisi Tanzania, tunasafiri tukijua kuwa tunakwenda kucheza na timu ambayo ni nzuri, lakini KMC FC  tunahitaji ushindi katika mchezo huo licha ya kwa mba tutakuwa ugenini, lakini tuna kumbukumbu nzuri katika mchezo uliopita.

 Hata hivyo KMC FC inasaka ushindi katika michezo miwili  Ugenini ambapo mbali na Polisi Tanzania, itakutana na Coast Union ya Jijini Tanga Jumapili  Machi saba katika uwanja wa Mkwawani. 



Bobi Wine ajipata 'mashakani kwa kuwa na gari la kifahari'


Kiongozi wa upinzani wa Uganda Robert Kyagulanyi, maarufu Bobi Wine amejipata mashakani kwa madai ya kuwa na gari ambalo haliingii risasi, kulingana na taarifa katika gazeti la Daily Monitor.

Gari hilo limevutia mamlaka nchini Uganda, huku mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru ya Uganda (URA) ikisema maelezo yaliyotolewa si sahihi na kwamba thamani yake iko chini kuliko inavyostahili kuwa.

URA, sasa inataka gari hilo kukaguliwa upya.

Bobi Wine, hata hivyo amekataa kuwasilisha gari hilo kwa misingi kwamba agizo hilo haliambatani na sheria, kulingana na taarifa yake iliyonukuliwa na gazeti la Daily Monitor.

“Japo mna uwezo chini ya kifungu cha 236(d) cha usimamizi wa forodhani katika Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC, kukagua bidhaa, hamna uwezo wa moja kwa moja kukagua tena bidhaa ambayo ilikuwa katika (bohari lenu), na ambayo ilikuwa imekaguliwa, kutathmini kodi na kodi hiyo kulipwa kabla ya bidhaa kutolewa kwa mmiliki/mlipa kodi," ilisema.

Gari hilo liliingizwa nchini na kusajiliwa Kenya mwaka jana na kisha kupelekwa Uganda kupitia mpaka wa Busia.

Katika ujumbe alioweka mtandaoni Februari 21, Bw. Kyagulanyi alidai kuwa gari hilo aina ya Toyota Land Cruiser lilitolewa kwake kama msaada na marafiki na wafuasi wake nchini Unganda na ughaibuni:



Rais wa zamani wa Ufaransa kujua hatma yake juu ya kesi ya ufisadi inayomkabili


Mahakama ya Ufaransa inatarajiwa kutoa uamuzi wake katika kesi ya ufisadi inayomkabili rais wa zamani Nicolas Sarkozy leo Jumatatu, huku waendesha mashtaka wakishinikiza muda zaidi gerezani kwa kiongozi huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 66. 

Sarkozy ambaye aliiongoza Ufaransa kutoka mwaka 2007 hadi mwaka 2012, anatuhumiwa kutoa nafasi ya kazi kwa jaji mmoja mjini Monaco kwa sharti kuwa angepata habari zaidi kuhusu uchunguzi juu ya fedha zake za kampeni.

 Rais huyo wa zamani ameiambia mahakama kuwa "hajawahi kufanya vitendo vyovyote vya ufisadi." Waendesha mashtaka wanataka apewe kifungo cha miaka minne jela na kutumikia angalau miaka miwili, na pia wanataka adhabu kama hiyo kwa washtakiwa wenzake-wakili Thierry Herzog na jaji Gilbert Azibert.



Okonjo-Iweala aanza rasmi kazi kama mkuu wa WTO


Dkt Okonjo-Iweala ni mwanamke wa kwanza Mwafrika kushikilia nafasi hiyoImage caption: Dkt Okonjo-Iweala ni mwanamke wa kwanza Mwafrika kushikilia nafasi hiyo

Mnageria-Mmarekani, Ngozi Okonjo-Iweala, anaanza rasmi kazi kama mkuu mpya wa Shirika la Biahsara Duniani (WTO) Jumatatu ya leo.

Dkt Okonjo -Iwela ambaye ni waziri wa zamani wa fedha na mambo ya nje wa Nigeria, ni mwanamke wa kwanza wa Afrika kuongoza WTO.

Ngozi Okonjo-Iweala amesema kipaumbele chake ni kushughulikia masuala ya afya na athari za kiuchumi zinazotokana na majanga.

Kuna wasiwasi huko Washington na miji mikuu mingine kuhusu sera za biashara za China na jinsi WTO inavyojiandaa kushughulikia masuala hayo.

Dkt Okonjo-Iweala anafahamika kwa kuwa mwana -mageuzi, lakini atakabiliwa na mslahi ya nchi wanachama.



Daktari Scott Green ajiunga na kesi kupitia Zoom huku akimfanyia mgonjwa upasuaji


Daktari mmoja, katika jimbo la California alijiunga na kesi ya uvunjifu wa sheria barabarani kupitia mtandao wa Zoom huku akimfanyia mgonjwa upasuaji.

Scott Green aliyekuwa amevalia mavazi ya kufanya upasuaji, tayari alikuwa katika chumba cha upasuaji wakati alipojiunga na mahakama kusikiliza kesi dhidi yake mtandaoni siku ya Alhamisi, Sacramento Bee iliripoti.

Alipoulizwa na jaji, Bw. Green alisema anaweza kuendelea na kesi, na kuongeza yuko na "mpasuaji mwingine ambaye anashirikiana naye".

Jaji alisema haitakuwa "sawa" na kuahirisha kesi.

Bodi ya Matibabu ya California imesema katika taarifa kwamba inachunguza kisa hicho, ikiongeza kuwa "anatarajia madaktari kufuata kanuni ya huduma wakati wa kutibu wagonjwa wao".

Kabla ya kusikizwa kwa kesi mbele ya Mahakama ya Juu zaidi ya Sacramento, ambayo ilioneshwa mubashara katika mtandao wa YouTube, karani wa mahakama alimuuliza daktari huyo: "Hujambo, Bw Green? Salama. Unapatikana kushiriki kesi hii? Inaonekana kana kwamba upo katika chumba cha upasuaji."

Green alimjibu: "Naam ni mimi, mkuu. Ndio, Niko katika chumba cha upasuaji muda huu. Naam, naweza kushiriki kwenye kesi. Endelea mbele."



Biden kutoa tamko kuhusu Saudi Arabia leo


Rais wa Marekani Joe Biden amesema leo Jumatatu, Machi 1, Serikali yake itatoa tamko juu ya Saudi Arabia kufuatia ripoti ya kijasusi ya Marekani kusema kuwa mrithi wa kiti cha Ufalme wa taifa hilo, Mohammed Bin Salman aliamuru mauaji ya muandishi habari Jamal Khashoggi.

Utawala wa Biden umekosolewa hasa katika ripoti ya gazeti la Washington Post iliyosema Biden angeonesha nguvu zake kwa Salman ambaye hakuwekewa vikwazo vya aina yoyote licha ya kutajwa kuhusika na mauaji ya Khashoggi.

Biden amesema atatangaza leo Jumatatu hatua watakayochukua kwa Saudi Arabia.

Jamal Khashoggi aliyekuwa uhamishoni Marekani akiandika ripoti zinazomkosoa, Mohammed Salman na Serikali ya Saudi Arabia, aliuwawa Oktoba 2, 2018, katika Ubalozi wa Saudi Arabia mjini Istanbul, Uturuki.



Afrika Kusini yaingia mkataba wa chanjo ya Covid na Johnson &Johnson


Afrika Kusini ndilo Taifa linapata changamoto kubwa barani Afrika kutokana na janga la Corona likirekodi nusu ya vifo vyote vya COVID-19 katika bara hilo na zaidi ya theluthi moja ya maambukizi yaliyoripotiwa katika bara zima la Afrika

Afrika Kusini imesaini mkataba na kampuni ya Johnson and Johnson ili kununua dozi millioni 11 za chanjo ya COVID-19 na italegeza masharti ya kupambana na janga la Corona kutokana na kupungua kwa kesi mpya, Rais Cyril Ramaphosa amesema Jana Jumapili.

Lakini maambukizi ya kila siku yalishuka chini ya elfu mbili kutoka kiwango cha elfu ishirini kwa siku kwa mwezi uliopita wakati wa wimbi la pili la maambukizi ya virusi vya corona.

Rais Ramaphosa amesema katika hotuba iliyopeperushwa kwenye televisheni kwamba dozi millioni mbili na laki nane za chanjo ya Johnson and Johnson zitatolewa katika robo ya pili na zilizobaki zitasambazwa baadaye mwaka huu.



Mwanangu akipata 'Division One' nampa Insta yangu - Nisha


Msanii wa filamu Nisha Bebe ametoa kali ya mwaka kwa kusema mtoto wake akipata 'Division One' atampa akaunti yake ya mtandao wa Instagram.

Nisha Bebe amesema ana mtoto wake wa kike mwenye umri wa miaka 16 na yupo kidato cha nne kwa sasa, hivyo ametumia njia hiyo kumpa nguvu kwenye masomo yake ili asiwe na vishawishi vingine, tamaa au ustaa ambavyo vitaharibu masomo yake.

"Mimi mtoto wangu hakuna mtu anayemjua ana miaka 16 yupo 'form four' hata shule watu hawajui anasoma wapi na nimeamua kuishi nae hivyo mpaka akifikisha miaka 18 ndiyo nitampost, nimemwambia akipata division one ya 7, nampa page yangu ya Instagram inakuwa ya kwake na jina nabadilisha" ameeleza Nisha Bebe



Simba kuzisaka pointi tatu katika mchezo wa leo dhidi ya JKT

 


DIDIER Gomes, Kocha Mkuu wa Simba amesema kuwa anatambua mchezo wa leo dhidi ya JKT Tanzania utakuwa na ushindani mkubwa ila amewaambia wachezaji wake wanapaswa kupambana ili kupata pointi tatu.

Mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Jamhuri, Dodoma, ubao ulisoma JKT Tanzania 0-4 Simba baada ya dakika 90.

Huku bao la kwanza la Luis Miquissone akiwa nje ya 18 likiwa ni moja ya bao bora na kushangilia kwa kuwafuata mashabiki kulimponza nyota huyo ambapo alionyeshwa kadi ya njano.

Gomes amesema:"Utakuwa mchezo mgumu ila tunahitaji pointi tatu muhimu,ushindi wetu ni mwanzo wa kuendelea kupunguza pointi ambazo tunadaiwa na wapinzani wetu.

"Ukweli ni kwamba kila timu ambayo tunakutana nayo ndani ya uwanja inafanya vizuri katika kusaka matokeo hivyo nasi kazi yetu ni kusaka ushindi,".

JKT Tanzania kwenye msimamo ipo nafasi ya 10 ina pointi 24 baada ya kucheza mechi 21 inakutana na Simba iliyo nafasi ya pili na pointi zake ni 42.




Waziri Mkuu wa Hungary achomwa chanjo ya China


Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban amechomwa Chanjo ya Sinopharm, iliyotengenezwa na China , dhidi ya virusi vya corona (Covid-19).

Orban amesema katika taarifa kwamba ilikuwa zamu ya maafisa wa serikali kupewa chanjo hizo na kwamba amechomwa wa kwanza yeye.

Akielezea kwamba alijisikia vizuri sana baada ya chanjo, Orban amesisitiza umuhimu wa chanjo katika wimbi la tatu la corona nchini humo.



Dismas Ten: Hakuna kama Haji Manara yeye ni msemaji kweli


 OFISA Habari wa zamani wa Klabu ya Yanga, Dismas Ten amesema kuwa kwake yeye ndani ya ardhi ya Tanzania Ofisa Habari bora kwenye vilabu vya soka Tanzania ni Hassan Bumbuli wa Yanga na Idrissa Bandari wa Ndanda FC. 

Ten amewahi kuwa Ofisa Habari wa Mbeya City na ndani ya Yanga amepitia nafasi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Kaimu Katibu.

Kupitia Ukurasa wake wa Instagram amesema kuwa kuna tofaiyi kubwa kati ya Ofisa Habari na Msemaji hivyo kwake msemaji bora ni Haji Manara ambaye ni Ofisa Habari wa Simba.

"Linapokuja suala la kuongeza, kuzungumza hakuna kama Haji Manara yeye ni msemaji kweli

"Ipo tofauti kati ya Ofisa Habari na msemaji,".



Chadwick Boseman ashinda tuzo ya muigizaji bora Golden Globe


Chadwick Boseman alishinda tuzo yake ya kwanza ya Golden Globe katika filamu ambayo hakuishi kuiona.

Mjane wa nyota huyo Taylor Simone Ledward, alikubali tuzo hiyo ya muigizaji bora kwa niaba ya muigizaji huyo , ambaye alifariki mwezi Agosti kutokana na saratani ya utumboakiwa na umri wa miaka 43 – miezi mitatu kabla ya filamu kwa jina ‘’Ma Rainey’s Black Bottom’’ kuzinduliwa.

‘’Angesema kitu kizuri chenye msukumo , kitu ambacho kingepaza ile sauti ndogo ndani yetu sote inayosema unaweza’’, alisema Simone Ledward, huku yeye na waliohudhuria wakijifuta machozi.

‘’Hilo linakwambia endelea, hilo linakuita na kukurudisha katika kile ambacho unapaswa kufanya wakati huu katika historia’’.

Boseman ni mtu mweusi wa kwanza katika orodha hiyo katika kipindi cha miaka 15.

Forest Whitaker alishinda katika sherehe ya 2007 kwa kuigiza kama Idi Amin ‘’the Last king of Scotland’’.

Tuzo hiyo pia inamfanya Boseman kuwa mtu mweusi wa kwanza aliyefariki kushinda tuzo hiyo katika orodha ya uigizaji.

Boseman alikuwa maarufu katika filamu ya michezo ya '42' ya mwaka 2013 kuhusu ubaguzi aliofanyiwa mchezaji wa kulipwa wa besiboli Jackie Robinson na ile ya 'Get on Up' mwaka 2014 kuhusu maisha ya mwimbaji wa nyimbo aina ya soul James Brown.

Nyota huyo, Boseman, aliigiza kama mtawala wa Wakanda, filamu iliyoangazia Afrika ya kufikirika yenye teknolojia zilizoendelea sana za kisasa.






Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...