
Hatimaye Samatta alitua Villa na sio Newcastle United. Kabla ya hapo alihusishwa pia kwenda Napoli ambayo ilimuona na kufurahia kiwango chake wakati wa mechi mbili za Ligi ya Mabingwa Ulaya kati ya Genk na Napoli.
Lakini pia Samatta alikuwa na nafasi ya kucheza Ujerumani kwa sababu mawakala wake wanatoka Ujerumani, na wanajuana na mabosi wa timu nyingi za kule. Hata hivyo, ndoto yake kubwa ilikuwa kucheza katika Ligi Kuu ya England.
Kwanini Aston Villa? usajili wa Januari siku zote ni mgumu. Timu huwa zinasajili wachezaji kwa ajili ya kuziba mapengo na upungufu uliojitokeza ndani ya kipindi kifupi tu tangu ligi ianze. Ndani ya miezi mitano tu kuna upungufu unakuwa umejitokeza.
Lakini pia uhamisho wa Januari unategemea zaidi nani anakwenda wapi ili nafasi ipatikane. Kwa mfano, Crystal Palace walimtaka Samatta, lakini hapohapo walikuwa wanasubiri kuona kama wanaweza kumnasa Olivier Giroud kwanza. Kama wakimkosa Giroud ndipo wamchukue Samatta.
Klabu zote za England zilitambua uwezo wa Samatta na zilithibitisha kwamba anaweza kucheza England, hasa baada ya kufunga mabao mawili ya kichwa dhidi ya Liverpool. moja lilikataliwa pale kwao Genk, jingine lilikubaliwa pale Anfield.
Kufa kufaana. Nafasi ya Samatta Villa imepatikana baada ya kuumia kwa Mbrazil Wesley Moraes. Huyu atakuwa nje mpaka mwishoni mwa msimu. Kinachoshangaza ni kwamba Wesley alinunuliwa na Villa akitokea Club Brugge ya Ubelgiji katika dirisha kubwa lililopita huku Samatta akiendelea kusota Genk.
Wesley alikuwa amefunga mabao 16 tu msimu uliopita pale Ubelgiji, lakini ni wazi kwamba kuna mambo matatu yalisababisha achukuliwe na Villa mbele ya Samatta. Kwanza ni Ubrazil wake, pili ni umri wake kuwa chini ya ule wa Samatta, lakini tatu Wesley ni mrefu na umbo lake linaonekana kufaa zaidi kwa Ligi Kuu ya England.
Hata hivyo, kwa nilivyowatazama Wesley pamoja na mshambuliaji wa Newcastle, Joelinton ambaye Newcastle waliamua kumchukua mbele ya Samatta, sioni ambaye ana uwezo mkubwa wa kumshinda Samatta. Lilikuwa suala la muda tu kabla ya Samatta kwenda England Januari. Muda tu.
Kitu kizuri zaidi kwa Samatta katika uhamisho huu ni kwamba mshambuliaji mwingine ambaye alikuwa anasaidiana na Wesley pale Villa, staa wa kimataifa wa Ivory Coast, Jonathan Kodja alikuwa anaonyesha kiwango kibovu na alipanga kuondoka Januari, na tayari ameshaenda Qatar.
Hii ina maana bado Samatta angeenda Villa hata kama Wesley angekuwa na miguu mizima. Nini kinafuata kwa Samatta? Nina uhakika kama atabakia kuwa na afya njema basi ataiteka Ligi kuu ya England bila ya wasiwasi.
Katika ligi hii ambayo inapendelea krosi za juu na chini, Samatta atawaonyesha yeye ni nani. Samatta ni mtaalamu sana wa mipira ya hewani na hapana shaka kwamba atafunga mabao mengi. Alishaonyesha katika mechi mbili za Ulaya dhidi ya Liverpool kwamba soka la England halitamsumbua kufunga mabao.
Kwa sasa ametinga England akiwa na umri wa miaka 27 lakini nampa mwaka mmoja na nusu kuondoka Aston Villa kwenda timu kubwa zaidi. Akiwa na umri wa miaka 27 Samatta bado ana umri sahihi wa kwenda timu kubwa zaidi.
Kuanzia sasa mpaka mwishoni mwa msimu anaweza kufunga mabao sita hadi saba, lakini kuanzia msimu ujao anaweza kufanya mambo makubwa zaidi. Kama Villa isiposhuka na Samatta akaenda katika mazoezi ya maandalizi ya msimu mpya (pre season) anaweza kufanya mambo makubwa zaidi.
Kwa kipindi hiki cha kuanzia sasa mpaka mwishoni mwa msimu atakitumia zaidi kuzoea mazingira. Kuanzia msimu ujao hatakuwa mgeni tena. Atawaonyesha yeye ni nani. Hata Genk ilikuwa hivyo hivyo. Hakuanza kwa kasi ambayo alimaliza nayo.
Katika msimu kamili kama akifunga mabao 15 tu, anaweza kupata dili la kwenda katika timu kama Chelsea, Arsenal, Manchester United na nyinginezo za kariba hiyo. Ni suala la kukimbizana na muda tu na wala sina hofu na Samatta.
Kitu cha msingi katika kikosi cha Villa ni kumlisha mipira tu. Juzi Samatta amecheza mechi yake ya kwanza dhidi ya Leicester katika pambano la nusu fainali michuano ya Carabao. Villa hawakumlisha vyema kwa sababu walicheza na timu ngumu ambayo iliwatawala. Alipoteza nafasi moja tu ya wazi lakini hakupata nafasi nyingi.
Katika mechi nyingine atapata nafasi nyingi na atafunga mabao mengi. Sio kila kitu ni Leicester. Watakuja akina Bournemouth na watakumbana na makali yake. Kila la heri kwa Mbwana Ally Samatta. Hii ndio safari yake ya kutoka Mbagala mpaka Aston Villa kwa kadri ninavyomfahamu.







































