Search This Blog

Saturday, October 23, 2021

Punguza kilo tano kwa siku saba

 


NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha maradhi mbalimbali bali pia mwonekano wako unakuwa si mzuri. Makala haya yanaeleza namna ya kupunguza unene ndani ya siku saba.

Siku ya 1: Asubuhi kula matunda (lakini usile ndizi). Mchana chemsha kabichi, weka chumvi kidogo na nyanya, chemsha na upate supu. Kula mchanganyiko huo na utajiona umeshiba. Jioni kula tikiti maji na mbogamboga au kabichi uliyotengeneza mchana.

Siku ya  2: Kula mboga za majani asubuhi (usile mboga za majani zenye wanga kama karoti).  Mchana kula kabichi iliyochemshwa, tengeneza na kachumbari. Katika kabichi weka chumvi, pilipili na mafuta ya olive.  Jioni unaweza kula mlo kama wa mchana lakini unaweza kukaanga mboga nyingine za majani.

Siku ya 3: Kula mboga za majani na matunda, unaweza kuongeza kiazi kitamu kimoja.

Siku ya nne 4: Kula ndizi moja na unywe na maziwa ya mtindi wakati wa asubuhi. Mchana kula kabichi kama ulivyoitengeneza kwenye siku ya kwanza, usiku rudia mlo wa mchana.

Siku ya  5: Kula nyanya nne pamoja na samaki au kipande cha kuku asubuhi. Mchana unaweza  kula samaki wa kuchemsha kiasi ambaye amechanganywa na nyanya.  Wakati wa jioni unaweza kula chakula kama cha mchana.

Siku ya 6:  Unaweza kula chakula cha protini na mboga za majani. Anza kwa kula kachumbari asubuhi. Mchana kula tambi kiasi na kipande kidogo cha samaki. Usiku tengeneza supu ya kabichi.

Siku ya 7: Anza kwa matunda na juisi. Mchana kula mboga za majani na usiku kula supu ya kabichi na kiazi kimoja.

Kumbuka: Unatakiwa kunywa maji angalau glasi nne kila siku. Usiendelee kwa muda mrefu, kumbuka dayati hii ni ni kwa siku saba. pekee.

Kitendawili cha Lissu, Lema kurejea Tanzania

 


Wakati Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema akidokeza mpango wake wa kurejea nchini kuendelea na siasa, makamu mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu amesema sababu zilizomfanya aondoke hazijaondoka bado zipo.


Kurejea kwa viongozi hao ambako kumeibuka mtandaoni huenda ukakiongezea nguvu chama hicho ambacho kwa sasa Mwenyekiti wake Freeman Mbowe yuko rumande akiendelea na kesi yake inayomhusisha makosa ya ugaidi.


Kutokuwepo viongozi hao mara kadhaa umetajwa kupunguza hamasa ya siasa kwa chama kikuu cha upinzani nchini na kusitisha programu zake kadhaa.


Hakikisho la Lema

Akizungumza juzi katika mitandao ya jamii, Lema aliyeondoka nchini baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 alisema anatafakari kufanya uamuzi wa kurejea Tanzania kuungana na ndugu zake, akisema majadiliano kuhusu hatua hiyo anayaanza hivi sasa.


“Nafanya uamuzi wa kuwepo Tanzania lini? Naanza sasa majadiliano na Mungu, familia na chama changu ili kufanya kazi pamoja. Nahitaji kuwa uwanjani (Tanzania) kuliko wakati wowote ule, nitakuwa tayari kukabiliana na matokeo yoyote,” alisema Lema.


Lema ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, alieleza hayo katika mtandao wa Club House unaowakutanisha wadau mbalimbali kwa ajili ya kujadili na kutoa maoni kuhusu mada inayowekwa mezani katika siku husika.


Kwa sasa Lema ambaye aliyekuwa mbunge wa Arusha Mjini anaishia nchini Canada alikopata hadhi ya ukimbizi wa kisiasa akitokea Nairobi, Kenya.


Katika mtandao huo, Lema alisema, “nafikiria nahitaji kumuona mwenyekiti (Freeman Mbowe) jela, akiwa mahabusu au mahakamani. Nahitaji kumtia matumaini, nahitaji vitu vingi kuhusu nyumbani, nipo tayari kwa lolote kabisa,” alisema Lema.


Lema aliwataka viongozi wa Chadema kusimama imara katika usimamizi wa kesi ya Mbowe, akisema mazingira ya kesi hiyo ni magumu.


Wakati, Lema akisema hayo, kiongozi mwenzake anayeishi nchini Ubelgiji Tundu Lissu alisema sababu zilizomkimbiza Tanzania kwenda ughaibuni bado hazijabadilika.


Lissu aliondoka nchini kwa mara ya kwanza Septemba 7, 2017 na kuelekea Nairobi, Kenya akiwa mahututi, baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana jijini Dodoma.


Mwaka 2018 alihamishiwa nchini Ubeligiji kwa matibabu zaidi hadi mwaka 2020 aliporejea nchini na kugombea urais, kabla ya kurejea tena Ubelgiji akidai kutishiwa maisha yake.


Akizungumzia hoja zilizoibuka mtandaoni baada ya mchungaji mmoja kuonekana akimkaribisha nyumbani, Lissu alisema “mtandaoni kuna Tundu Lissu wengi, huyo anayeelezwa na pastor (jina tunalihifadhi kwa sababu hatukumpata), sio yule Tundu Lissu aliyeko uhamishoni.


Alipotakiwa kufafanua kauli yake, Lissu alisema: “Sababu zilizonikimbiza Tanzania hazijabadilika. Wauaji bado wako huru mitaani na hakuna mpango wa kuwatafuta na kuwashughulikia kwa mujibu wa sheria.’’



Songwe kuwasaka watoto 1,000 waliokimbia shule

 


Mkuu wa wilaya ya Songwe, Simon Simalenga amesema wamejipanga kuanzisha oparesheni ya kuwasaka watoto zaidi ya 1,000 ambao hawafiki shuleni ili kukomesha tatizo la utoro kwenye shule za msingi zilizopo katika halmashauri ya Songwe mkoani Songwe.


Simalenga ametoa kauli hiyo Oktoba 21 kwenye kikao cha baraza la madiwani cha robo ya kwanza katika mwaka wa fedha 2021/22


Amesema atahakikisha wazazi wa watoto hao wanasakwa ili waweze kuwahamasisha watoto wao kuendelea na masomo.


“Siwezi kukubali watoto zaidi ya 1,000 kutofika shule lazima wazazi wa watoto hawa wafuatiliwe ambapo amesema atahakikisha watoto wote wanaozurura wanakamatwa na kurudishwa shuleni,” alisema Simalenga.


Simalenga amewaomba madiwani wa halmshauri hiyo kuhakikisha wanakaa na wazazi na kuwaeleza umuhimu wa elimu ili kukomesha suala la utoro na kujenga taifa lililo salama kwamadai mtoto anapokuwa mtaani hujiingiza kwenye makundi hatarishi.


Ofisa elimu wa shule za msingi katika halmashauri ya Songwe, Michael Nzunda amesema tatizo la utoro sugu kwenye shule za msingi zilizopo katika halmshauri hiyo umetajwa kuwa ni moja ya changamoto inayochangia kushuka kwa kiwango cha elimu wilayani humo na kwamba wanaendelea kuchukua hatua mbalimbali kudhibiti hali hiyo.


Nzunda amesema tayari wamewarejesha shuleni watoto 200 na kwamba wanaendelea kuwafuatilia watoto 1,000 ili waweze kuendelea na masomo.


Ofisa huyo alibainisha sababu tano zinazochangia tatizo la utoro katika halmashauri hiyo kuwa ni shughuli za uchimbaji madini ya dhahabu, ufugaji, uvuvi, umbali wa shule ambapo amesema baadhi ya watoto hutembea umbali wa zaidi ya kilometa 15 kufuta shule.


Philipo Mulugo ambaye ni mbunge wa jimbo la Songwe, alisema amesikitishwa na idadi hiyo ya wanafunzi hao kutofika Shule ambapo amesema atahakikisha anaungana na mkuu wa wilaya katika kukomesha tatizo hilo la utoro kwa halmashauri ya Songwe.



Mashambulizi ya jeshi la Ethiopia Tigary yazuia ngege ya misaada kutua

 


Mashambulizi ya anga ya jeshi la Ethiopia katika mji mkuu wa jimbo la kaskazini la Tigray, yamesababisha ndege ya misaada ya Umoja wa Mataifa kushindwa kutua mjini Mekelle. 


Kwa mujibu wa taarifa ya afisa mratibu wa misaada ya dharura wa Umoja wa Mataifa, Martin Griffths tukio hilo lilitokea jana, Ijumaa na kwamba ndege husika ilirejea mjini Addis Ababa.


Griffths aliongeza kwa kusema tukio hilo linaongeza wasiwasi mkubwa kuhusu usalama wa wafanyakazi wenye dhima ya kutoa misaada ya kiutu katika kusaida raia wenye uhitaji.


Hata hivyo Umoja wa Mataifa ulikuwa na kibali cha safari ya ndege hiyo na haukupata tahadhari ya onyo la mashambulizi ya Makele. Takribani mwaka mmoja tangu kuanza kwa mzozo wa Tigray, kiasi ya watu 400,000 wanakabiliwa na kitisho kikubwa cha njaa, katika eneo hilo la kaskazini mwa Ethiopia.



Hawa Waethiopia wamekula chakula chetu sasa - RPC

 


Jeshi la Polisi mkoa wa Njombe linawashikilia raia 52 kutoka nchi za Ethiopia na Malawi wanaodaiwa kuingia nchini bila ya kufuata utaratibu wakijaribu kuvuka mipaka kuelekea nchini Afrika Kusini.


Akizungumza mara baada ya kuwakamata raia hao, Kamanda wa Polisi mkoa wa Njombe, Khamis Issah, amesema kuwa watu hao wameharibu tu bajeti ya Taifa, kwani wamekula chakula ambacho hakikuwa kwenye bajeti yao.



Rais wa Burundi awasili visiwani Zanzibar


Na THABIT MADAI, ZANZIBAR

 

RAIS wa Jamuhuri ya Watu wa Burundi, Jenerali Evariste Ndalishimiye amewasili kwa Mara ya Kwanza Visiwani Zanzibar, Ikiwa ni Muendelezo wa ziara yake ya Siku Tatu Nchini Tanzania.

 

Mara baada ya kuwasili Visiwani humo Rais Ndalishimiye na Ujumbe wake toka Burundi wamepata fursa ya kuzungumza na Mwenyeji wao Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Ali Mwinyi, Ikulu Mjini Unguja.

 

Katika Mazungumzo hayo Rais wa Zanzibar Dkt Hussein Ali Mwinyi amempongeza Rais wa Burundi kwa kuhakikisha anasimamia ya Nchi ya Burundi suala la Amani toka aingie madarakani.

 

“Nikupongeze kwa kuhakikisha kuwa unasimamia suala zima la Amani ya Wananchi wa Burundi toka uingie madarakani,”alisema

 

Dkt Mwinyi alimueleza kuwa Viongozi wa Tanzania wanaendelea kumuombea katika kuongoza Nchi kwa Amani na Utulivu.

 

 

Pia alisema kuwa Zanzibar ni sehemu ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania hivyo atahakikisha anaunga mkono harakati za kuimarisha uchumi wa Tanzania na Burundi.

 

“Nikuhakikishie kuwa naunga mkono jitihada za kuimarisha uchumi wan chi zetu,”alisema.

 

 

Kwa upande wake, Rais Jamuhuri ya Burundi Jenerali  Evariste Ndalishimiye alipongeza namna Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa namna ya wanavyyonga Nchi kwa kuzingatia msingi ya Utawala bora.

 

 

“Sisi kama warundi tunajifunza mengi kutoka Tanzania hivyo niwapongeze hasa Rais Samia Suluhu Hassani kwa namna anavyoiongoza Tanzania,”alieleza.

 

 

Katika Hatua nyingine Rais Ndalishimiye, aliishukuru Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwapokea raia Burundi wakati wa machafuko ya wao kwa wao.

 

 

Kwa upande wao Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Libarata Mulamula alisema kuwa ziara hiyo imekuja kuongeza ushirikiano baina ya Tanzania na Burundi.

 

“Ziara hii imekuja kuunganisha sana n asana Tanzania na Burundi,”alisema

 

 

Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora Haroun Ali Suleiman amesema kuwa Rais wa Burundi kupitia ziara hiyo amevutika sana kuja kuwekeza Zanzibar katika miradi mbalimbali ya Maendeleo.

 

 

Katika Ziara hiyo Rais Evariste Ndalishimiye alipata fursa ya kutembelea miradi mbalimbali ya Maendeleo pamoja na sehemu za kihistoria huku Mwenyeji wake Rais Dkt Mwinyi alimuandalia hafla maalum ya Chakula cha Mchana Ikulu Visiwani Zanzibar.

 

 



Ndalichako aagiza kila Mtendaji wa Wizara na Taasisi zitakazotekeleza miradi fedha za UVIKO 19 kukamilisha ifikapo Octoba 30


Na Ezekiel Mtonyole – Dodoma.

Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe. Profesa Joyce Ndalichako amewaagiza watendaji wa Wizara na taasisi zitakazotekeleza miradi ya fedha za mpango wa maendeleo  kwa ustawi wa taifa na mapambano dhidi ya uvico 19, hadi kufikia Octoba 30, 2021 wawe wamekamilisha mpango na maandalizi ya utelelezaji wa miradi hiyo.

Waziri Prof. Ndalichako ameyabainisha hayo leo Octoba 23, 2021 jijini Dodoma wakati akitoa mchanganuo wa fedha zitakazotekeleza miradi ya fedha hizo miradi ambayo ipo chini ya Wizara ya Elimu ambapo amebainisha kuwa kwa sekta ya Elimu imetengewa bilioni 368.9 na Wizara ya Elimu imepata shilingi bilioni 64.9 kutekeleza miradi iliyochini ya Wizara hiyo.

Ambapo Waziri Ndalichako amesema hadi ifikapo Octoba 30, 2021 kila taasisi itakayotekeleza mradi huo iwe imekamilisha maandalizi na mipango ya utekelezaji ikiwa ni pamoja na kuandaa mpango kazi utakao ainisha hatua mbalimbali za taratibu za manunuzi ya huduma na vifaa.

“Hadi tarehe 30 mwezi huu kila taasisi iwe imekamilisha na iainishe lini vifaa vitanunuliwa, vifaa vyote vinunuliwe kwa kuzingatia bei ya soko nataka na mimi nikienda kununua kifaa bei iwe ndio hiyo” amesema Prof. Ndalichako.

Aidha ameagiza miradi hiyo kuhakikisha inakamilika kabla au ifikapo May 30, 2022 na kusisitiza matokeo ya utekelezaji wa mradi yaendane na thamani ya fedha zilizotolewa na si vinginevyo.

Ameongeza kuwa “Namuagiza Katibu Mkuu wa Wizara aandae mfumo wa uratibu, usimamizi na ufuatiliaji wa miradi utakao wezesha kubaini changamoto zitakazo kuwa zikijitokeza na kuchukua hatua stahiki na kwa wakati” amesema.

Pia ametahadharisha kwamba fedha hizo hazihusishi ulipanaji wa posho ya aina yoyote na viongozi wa taasisi zinazohusika na kwamba yeye atafuatilia kwa ukaribu katika utekelezaji wa miradi hiyo.

Amebainisha kuwa fedha hizo zitakwenda kuimarisha ufundishaji kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu ambapo shilingi bilioni 1.47 zimetengwa, kuimarisha elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stedi ambapo kiasi cha shilingi bilioni 57.98 zimetengwa na kuimarisha mazingira ya utoaji elimu ya ualimu ambapo kiasi cha shilingi bilioni 5.44 zimetengwa.

 



Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...