Utawala wa Rais wa Marekani Joe Biden umesema unaridhia kufanya mazungumzo na Iran juu ya makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015 licha ya Iran kukataa mualiko wa Umoja wa Ulaya kujiunga na mkutano na Marekani na washirika wengine kwenye makubaliano hayo.
Afisa mmoja mwandamizi amesema Marekani imehuzunishwa na hatua ya Iran kukataa mualiko huo. Afisa huyo mwandamizi amesema Marekani itashauriana na washirika wengine ambao ni Uingereza, China, Ufaransa, Ujerumani, Urusi na Umoja wa Ulaya juu ya hatua zaidi za kufanya.
Afisa huyo haruhusiwi kuzungumia juu ya suala hilo na alifanya hivyo kwa sharti la kutotambulishwa. Mapema Jumapili, Iran ilikataa ofa ya mazungumzo ikisema kuwa sio wakati sahihi kwa mkutano huo, mkutano ambao Marekani ingeshiriki kama muangalizi.
Iran imekuwa ikisisitiza kuwa Marekani inafaa kuondoa au kulegeza vikwazo ilivyowekewa na utawala uliopita wa Donald Trump chini ya kampeni yake ya kuiwekea mbinyo Iran.

No comments:
Post a Comment