Na Ahmad Mmow, Lindi.
Wakulima wanaouzia korosho zao katika chama kikuu cha ushirika cha Lindi Mwambao, mkoani Lindi leo wamegoma kuuza.
Wakulima hao wamegoma kuuza katika mnada huo wa kwanza kwa chama kikuu cha Lindi Mwambao kwa msimu wa 2021\2022 ambao umefanyika katika kijiji cha Nachunyu.
Wakulima hao ambao waliwawakilisha wakulima wenzao waliopo katika wilaya za Lindi na Kilwa waligoma baada ya kutoridhika na viwango vya bei vilivyofikiwa na wanunuzi.
Katika mnada huo jumla ya tani takribani 1400 za korosho ghafi zilitarajiwa kununuliwa.
Hata hivyo wakulima walikataa kuuza kwa bei zilizoombwa na kampuni 12 zilizojitokeza kwenye mnada huo.
Bei ya juu kwa kila kilo moja ambayo wakulima wamegomea ni shilingi 2,275. Ambapo bei ya chini ilikuwa shilingi 2,010.
Wakulima hao waligoma baada ya maofisa wa idara ya ushirika kutangaza bei za juu zilizofikiwa na waombaji.
Ambapo mwenyekiti wa Lindi Mwambao, Ismail Nalinga aliwahoji wakulima mara tatu kama walikuwa tayari kuuza kwa bei hizo ambazo zilitokana na ushindani wa kampuni hizo 12.
" Ndugu wakulima wenzangu, wataalamu wamekokotoa na kutueleza bei za juu ambazo zimeombwa. Sasa mpo tayari na mnakubali kuuza kwa bei hizo?," aliuza Nalinga, huku wananchi wakimjibu hatuuziiiii.
Kufuatia hali hiyo mkuu wa wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga ambae alimwakilisha mkuu wa mkoa wa Lindi, Zainabu Telack aliwaasa wakulima wawe watulivu na kwamba uamuzi wao unaheshimiwa.
Ndemanga alisema kutokanana korosho hizo kushindwa kununuliwa kupitia mnada huo, itapangwa tarehe nyingine ya kunadi korosho hizo.
Msimu wa ununuzi wa korosho ghafi kwa msimu wa 2021\2022 ulipangwa kuanza 2.10.2022.
Ambapo mnada wa kwanza kwa chama hicho ungefanyika tarehe hiyo. Hata hivyo haukufanyika kutokana na makusanyo madogo.
Wakati hali ikiwa hivyo katika chama kikuu cha Lindi Mwambao, bado haijafahamika chama kikuu cha ushirika cha RUNALI kitafanya lini mnada wake wa kwanza kwa msimu huu wa 2021\2022. Sababu ikitajwa ni makusanyo madogo ya korosho.
No comments:
Post a Comment