Iran imeiomba Marekani kuzifungua baadhi ya akaunti zake za benki ilizozifungia kama ishara ya nia njema kwa ajili ya kufufuliwa mchakato wa majadiliano ya nyuklia mjini Vienna.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Iran Hossein Amir Abdollahian, amesema ikiwa Marekani ina nia ya kweli kuelekea majadiliano hayo basi inapaswa kuachia dola bilioni kumi za Iran zinazozuiliwa katika akaunti za benki katika nchi za nje.
Majadiliano ya kuyaokoa makubaliano ya nyuklia ya Iran yaliotiwa saini mwaka 2015 mjini Vienna, yalioanzishwa tena mwezi Aprili, yaliahirishwa baada ya uchaguzi uliofanyika mwezi Juni Iran na mabadiliko ya serikali nchini humo.
China, Ujerumani, Ufaransa, Uingereza na Urusi zinataka kuirejesha Marekani katika makubaliano hayo na pia kuitaka Iran kuyaheshimu baada ya kuyakiuka mara kadhaa tangu Marekani ilipojiondoa mwaka 2018 ikiwa chini ya rais wa zamani Donald Trump.

No comments:
Post a Comment