Hakimu mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Amalia Mushi aliahirisha hukumu hiyo Oktoba Mosi mwaka huu, baada ya Hakimu mkazi Mwandamizi Odira Amworo, kutokamilisha kuandika hukumu hiyo.
Hakimu Mushi aliahirisha hukumu na kusema kuwa itatolewa leo Oktoba 15 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.
Agosti 24 mwaka huu, Sabaya na wenzake Sylvester Nyegu na Daniel Mbura walikamilisha kujitetea mahakamani hapo baada ya Jamhuri kukamilisha mashahidi 11 na vielelezo vinane.
Sabaya alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Juni 4, mwaka huu baada ya kukamatwa Mei 27 wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Watuhumiwa hao walipandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka matatu ya unyang’anyi wa kutumia silaha .
Awali, kesi ya Sabaya na wenzake ilikuwa inatajwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Salome Mshasha lakini, Julai 16, Hakimu Amworo kutoka Geita alikuja Arusha kusikiliza kesi hiyo na ilianza mfululizo kuanzia Julai 18 mwaka huu hadi Agosti 24.
Agosti 12 watuhumiwa hao walielezwa kuwa wana kesi ya kujibu baada ya kukamilika ushahidi wa mashahidi 11 wa Jamhuri na vielelezo vinane.
Washtakiwa hao walikuwa wakitetewa na mawakili Dancan Oola, Mosses Mahuna, Edmund Ngemela, Sylvester Kahunduka, Fridolin Gwemelo na Jeston Jastin.
Upande wa Jamhuri ulikuwa ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu Tumaini Kweka, Wakili wa Serikali Mwandamizi Abdallah Chavula na mawakili wa serikali Felix Kwetukia na Baraka Mgaya.
No comments:
Post a Comment