Umoja wa Ulaya umesema haukuarifiwa kuhusu kuundwa kwa ushirika mpya wa kijeshi kati ya Marekani, Uingereza na Australia, kabla ya kutangazwa kwa mkataba wa ushirika huo, ikiwa ni kwa mujibu wa msemaji wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Peter Stano.
Hali hiyo inazidisha wasiwasi kuwa Marekani inaitenga Ulaya katika masuala ya usalama. Msemaji huyo amesema watajaribu kuzungumza na Marekani, Uingereza na Australia ili kujua kinachoendelea, na kuwa nchi za Ulaya zitajadiliana kuhusu athari ya uamuzi wa nchi hizo tatu.
Viongozi wa nchi hizo washirika, rais wa Marekani Joe Biden, waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson na waziri mkuu wa Australia Scott Morrison waliutangaza ushirika huo jana katika kile kinachotafsiriwa kama hatua ya kukabiliana na ushawishi wa China unaozidi kupanuka katika ukanda wa Indo-Pasifiki.
Awali China iliukosoa vikali ushirika huo uliopewa jina la AUKUS, ikiutaja kuwa wenye kukosa umakini, na ulio na malengo ya kuhujumu utengamano wa kikanda.

No comments:
Post a Comment