Search This Blog

Sunday, September 5, 2021

Serikali ya Indonesia yaipongeza serikali ya Tanzania, yaahidi kupiga jeki chuo cha ufundi

 


Na Ahmad Mmow, Lindi.

Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imepongezwa kwa jitihada yake ya kuwapa ujuzi vijana kupitia vyuo vya mafunzo ya ufundi stadi na huduma(VETA).

Pongezi hizo zimetolewa leo mjini Lindi, na balozi wa Indonesia nchini Tanzania, Profesa Ratlan Pardede baada ya kutembelea chuo cha mafunzo ya ufundi stadi na huduma kilichopo katika manispaa ya Lindi.

Profesa Perdede alisema serikali imefanya jambo jema na kubwa kujenga vyuo hivyo ambavyo vinatoa ujuzi kwa vijana ambao unawaingiza kwenye soko la ajira moja kwa moja.

Alisema juhudi hizo zimeanza kuzaa matunda. Kwani vimeanza kuzalisha vijana wenye ujuzi, ambao wanatengeneza bidhaa nzuri na bora ambazo zinaweza kutoa ushindani mkubwa sokoni.

Katika hali iliyodhihirisha balozi huyo amefurahishwa na aliyoyaona chuoni hapo ameahidi kuzitangaza bidhaa aliziona katika chuo hicho. Ikiwemo bidhaa zinazotokana na nguo.

Alisema vyuo hivyo vinanafasi kubwa ya kuzalisha vijana wenye ujuzi ambao wanaweza kutumika kwenye mradi wa kuchakata gesi asilia ambao unatarajiwa kutoa ajira nyingi kwa wananchi. Hasa wanaoishi katika mikoa ya Lindi na Mtwara.

Kwa kuzingatia ukweli huo balozi Pardede ameahidi serikali ya Indonesia kupeleka wataalamu ambao watatoa mafunzo kwenye chuo hicho. Lakini pia akiahidi kutengeneza ushirikiano baina ya vyuo vya VETA na vyuo vya ufundi vilivyopo nchini Indonesia.

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Lindi, Zainabu Telack licha ya kumshukuru balozi Pardede kutembelea mkoa huu lakini pia alisema litakuwa jambo jema iwapo Indonesia itasaidia wataalamu watakao toa mafunzo kwa wananchi ili waweze kuwa na ujuzi wa kutengeneza bidhaa zinazotokanana mazao yanayozalishwa katika mkoa huu.

Alisema kwakufanya hivyo mazao yanayo zalishwa katika mkoa huu na nchini kwa ujumla yataongezewa thamani na kumudu ushindani sokoni. Badala ya kuuza yakiwa ghafi. 

Aliyataja baadhi ya mazao hayo kuwa ni korosho na ufuta. Ikiwa ni miongoni mwa mazao ya kilimo ya biashara  yanayo zalishwa kwa wingi mkoani humu.

Teleck pia alitoa wito kwa wakezaji kuja kuwekeza mkoani Lindi katika sekta mbalimbali za kiuchumi. Kwani ni miongoni mwa mikoa yenye fursa nyingi kwa wawekezaji.

Nae ofisa katika wizara ya mambo ya nje, Afrika ya Mashariki na ushirikiano wa Kikanda anaesimamia nchi 11 za Asia Mashariki, Luangisa   Emmanuel alisema ziara hizo na idadi kubwa ya wawekezaji wanao wekeza nchini, watalii wanaokuja kutalii na ushirikiano wenye tija baina ya Tanzania na mataifa mengine ni juhudi za serikali kupitia wizara hiyo.

Maeneo mengine yaliyotembelewa na balozi huyo ni kivuko cha Kitunda, mashamba ya chumvi na minazi.



No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...