Ni simulizi isiyopendeza kuisikia baada ya familia moja kupoteza watu wanane ndani ya siku 10, huku sita wakizikwa leo kufuatia ajali iliyotokea juzi jijini Mbeya.
Ajali hiyo ilitokea wakati wanafamilia hao wakirejea kutoka kumzika mwanafamilia mwingine aliyefariki Septemba 15.
Kati ya watu hao wanane, watano walifariki juzi asubuhi na mmoja alifariki mchana wakati akiendelea kupatiwa matibabu na kuongeza idadi ya waliofariki kufikia sita ambao wote kwa pamoja watazikwa leo kwenye makaburi ya familia Vwawa mkoani Songwe.
Awali Septemba 13 familia hiyo ilipoteza mwanafamilia mwingine aliyefariki na kuzikwa jijini Dar baada ya kuugua.
Akizungumza na Mwananchi jana, mmoja wa wanafamilia hao, Gamariel Mboya alisema wamepata pigo kubwa kutokana na vifo hivyo lakini wanaamini ni mapenzi ya Mungu.
Alisema: “Hawa Joyce na Isabela walisafiri na wanafamilia wengine kwenye coaster ambayo ilikwenda Mbeya na kurudi Dar baada ya mazishi, kwa kuwa walimuona kaka yao amekuja na gari binafsi wakaona si vibaya kuongozana naye wakati wa kurudi,” alisema Mboya na kuongeza:
“Kwenye lile gari dereva alikuwa Thomas, ambaye alikuwa na mtoto wake Erick, alikuwepo pia mama mdogo na hao dada wawili,” alisema Gamariel.
Familia imepata pengo
Alisema kuwa waliofariki walikuwa washiriki kwenye matukio mbalimbali ya familia hivyo wameacha pengo kubwa.
Gamariel alisema siku chache kabla ya kukumbwa na mauti, Joyce alikuwa akiwasisitiza wanafamilia kujiweka karibu na Mungu na kutanguliza maombi.
“Tukiwa kwenye msiba wa mjomba uliotokea Septemba 13, dada Joyce alitusisitiza kuhusu maombi na umuhimu wa kujiweka karibu na Mungu, hata dada Isabela ndiye aliyebeba msalaba wa shangazi kule Mbeya wakati tunatoka nyumbani kwenda kuzika.”
Katika hatua nyingine Gamariel alitoa wito kwa Serikali kuzifanyia ukarabati na kuweka mkakati maalumu wa kupunguza ajali kwenye maeneo korofi ya barabara yanayosababisha ajali za mara kwa mara.
Alisema: “Hilo eneo ajali zimekuwa zikitokea mara kwa mara hivyo kuna umuhimu wa kuwepo mikakati ya dhati ya kuzikomesha, tumeona maisha ya watu yanakatishwa,” alisema.
Ajali ilikuwaje
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Urlich Matei, ajali ilitokea asubuhi ya Septemba 21 katika kijiji cha Imezu kata ya Inyala wilayani Mbeya vijijini.
Alisema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa gari lingine ambaye hakuchukua tahadhari wakati akilipita Lori aina ya Scania lililokuwa limepata hitilafu barabarani likiwa na mzigo wa kokote kwa kuligonga kwa nyuma na kwenda kuligonga gari lililowabeba wanafamilia hao.
Watu watatu walifariki papo hapo, wengine watatu walifariki wakipatiwa matibabu Hospitali ya Mkoa wa Mbeya.
Waliofariki ni Thomas Mboya ambaye ni askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na mkazi wa Morogoro, Isabella Mboya (Dar), Magreth Mwaisaka, Severine Mgalla na Joyce Mboya, wakazi wa Mbozi na Erick Mboya.

No comments:
Post a Comment