Na Ezekiel Mtonyole, Mbeya.
Zaidi ya shilingi bilioni 16 zitatumika katika ukarabati na ujenzi wa miondombinu mipya katika chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) ikiwa ni jitihada za Serikali katika kuhakikisha inaboresha elimu hasa katika nyanja za Sayansi na teknolojia na kuongeza udahili kwa wanafunzi.
Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia tayari imepeleka kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya ujenzi wa Maktaba, Hosteli, ununuzi samani na vifaa vya kisasa vya kufundishia na kujifunzia katika chuo hicho.
Akizungumza na Waandishi wa habari waliofika katika chuo hicho kwa ziara ya kutembelea uboreshwaji wa miondombinu unafanywa na Wizara ya Elimu katika vyuo na shule hapa nchini, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo hicho anaesimamia Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu chuoni hapo Profesa Godliving Mtui amesema wanaishukuru Wizara hiyo kwa kutoa fedha hizo.
Amesema mwaka 2019 walitembelewa na aliyekuwa Rais wa Tanzania,marehemu Dkt John Magufuli ambapo aliweka jiwe la msingi la ujenzi katika mradi wa Maktaba ambayo ina uwezo wa kuchukua wanafunzi 2500 kwa wakati mmoja.
Amesema gharama za ujenzi wa maktaba hiyo ni zaidi ya shilingi bilioni 5 ambapo mradi huo umegawanyika katika awamu mbili.
“Hapa Must tuna bahati tulitembelewa mwaka juzi na aliyekuwa Rais Dk. John Magufuli pamoja na mambo mengine aliweka jiwe la msingi katika mradi wa Maktaba mpya ni kubwa inaweza kuwa na watumiaji 2500, kwa ukanda huu ukiacha ile cha Chuo Kikuu cha Dar es salaam hakuna zaidi ya hii na Mheshimiwa Rais kuna fedha alielekeza zije.
“Kwenye Maktaba ile kuna upande wa kwanza ambao imeishakamilika na kuna samani ambazo tumeanza kuzifunga.Awamu zote mbili za ujenzi wa maktaba hiyo zimetumia shilingi bilioni tano kwa maana ya ujenzi na kuweka samani, huu ni mradi wa kujivunia” amesema Prof.Mtui
Vilevile,amesema Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, imetoa shilingi bilioni 10.9 kwa ajili ya kuboresha maabara na ununuzi wa vifaa vya kisasa kwa ajili ya karakana.
“Kama nilivyosema hiki chuo kilijengwa mwaka 1980 kwa hiyo miundombinu yake imeanza kuchakaa Serikali imetoa fedha kwa ajili ya kufanya maboresho ambapo jumla ya shilingi bilioni 10.9 tumezipata kwa ajili ya ununuzi wa vifaa,”amesema.
Amesema kwa sasa tayari wameishapata mkandarasi na kwa ajili ya kufunga vifaa hivyo ambapo amesema kuna baadhi ya vifaa vipo bandarini na vingine vipo njiani vinakuja.
“Lengo ni kuwa na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia chenye vifaa vya kisasa katika karakana zake katika studio zake ni kwa ajili ya usanifu na ukadiriaji,”amesema.
Pia amesema kuna mradi mwingine wa ujenzi wa Hosteli za wanafunzi ambazo zina uwezo wa kuchukua wanafunzi 1000 ambapo amedai hayo ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais mara baada ya kuelezwa changamoto hiyo alipofika chuoni hapo.
“Mradi huu tunajenga majengo yetu kwa utaratibu wa ndani miradi mingi tunafanya wenyewe kwa sababu tuna uwezo,”amesema.
Vilevile, amesema wamepatiwa milioni 750 kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi za watumishi ambao amedai wameweza kujenga ofisi 84 kwa ajili ya watumishi hao.
“Nichukue fursa hii kuishukuru sana Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Niseme tumejenga madarasa mawili pacha kwa kutumia fedha za ndani sio tu tunategemea serikali tu hata sisi tunajenga kwa kutumia ada na ushauri wa kitaalamu tunaotoa, tunafanya vitu vya maendeleo kila jengo lina uwezo wa kuchukua wanafunzi 400.
“Nichukue nafasi hii kuishukuru Serikali kwa kuipa kipaumbele Must baada ya msaada huu chuo hichi kitapaa na kuwa cha Kimataifa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alikuwa na ndoto hiyo kuhudumia ukanda wa SADEC,” amesema.
Nao baadhi ya wanafunzi wanaosomeshwa na Serikali kozi mbalimbali za ufundi wameishu kuruka Serikali kwa kuweka mpango huo kwani umewasaidia kupata ujuzi utakaosaidia wao kujitegemea mara baada ya kumaliza kozi hizo.
"Tunaishukuru sana Serikali maana wengi wetu tulikuwepo tu mtaani lakini tukasikia kuna kozi zinatolewa bure tukajitokeza na sasa tunapata ujuzi bure kabisa na hakuna upendeleo katika uchaguzi" amesema Rozaria.
|
|||

No comments:
Post a Comment