Maelfu ya watu wameandamana katika mji mkuu wa Ufaransa Paris na katika miji mingine nchini humo dhidi ya pasi maalumu kuhusu virusi vya corona.
Maandamano mengi yalikuwa ya amani lakini baadhi ya waandamanaji mjini Paris walikabiliana na polisi wa kukabiliana na ghasia waliowafyatulia gesi za kutoa machozi.
Mvutano uliibuka mbele ya kilabu maarufu cha Moulin Rouge huko Kaskazini mwa Paris katika kile kilichoonekana kuwa maandamano makubwa zaidi.
Polisi waliokuwa wakishika doria katika eneo hilo mara kwa mara walikabiliana na waandamanaji hao kwa kutumia ngumi.
Huku viwango vya maambukizi ya virusi vya corona vikiongezeka, wabunge nchini humo wamepitisha muswada unaohitaji pasi hiyo maalumu katika maeneo mengi ifikapo Agosti 9.
Pasi hiyo inahitaji mtu awe amepata chanjo ama kufanya upimaji wa haraka wa kuthibitisha kutokuwa na maambukizo na pia kuhimiza chanjo ya lazima kwa wahudumu wote wa afya kufikia katikati mwa mwezi Septemba.

No comments:
Post a Comment