Maofisa kutoka idara ya ardhi Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero wamenusurika kifo baada ya baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Melela kata ya Chita halmashauri ya Wilaya ya Mlimba kushambulia gari la mkurugenzi wa hamalshauri hiyo walilokuwa wakitumia na kulichoma moto pamoja na pikipiki.
Inadaiwa wananchi hao walichukua uamuzi huo baada maofisa hao kufika kwenye shamba la mwekezaji ambaye anadaiwa kwa muda mrefu hajaliendeleza shamba hilo.
Inadaiwa wananchi walivamia shamba hilo na kuanza kuishi zaidi ya miaka 20 sasa.
Maofisa hao walipofika walitaka kufanya upimaji ndipo wakavamiwa na gari kuwashambulia na kuchomwa moto.
Akizungumza kwa njia ya simu na Mwananchi, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Hanji Godigodi alikiri kuwepo kwa tukio huku akieleza kuwa kwa sasa ametoka kwenye mwenge hivyo awezi kuzungumzia hivyo atafutwe Mkuu wa Polisi Wilaya(OCD) na yeye atalizungumzia tukio hilo kesho.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Fortunatus Muslimu alipopigiwa simu kuzungumzia tukio hilo alisema “Ni kweli tukio hilo lipo na mkuu wa upelelezi mkoa yuko eneo la tukio akiendelea na kamatakamata taarifa zaidi nitatoa baadae."

No comments:
Post a Comment