Waasi katika jimbo la Tigray nchini Ethiopia wamesema ili wasitishe mapigano katika eneo hilo, ni sharti watambuliwe kama serikali halali.
Kuondolewa kwa majeshi ya Eritrea katika eneo hilo, pia ni moja ya sharti.
Hapo awali mamlaka mjini Addis Ababa zilieleza kusitisha mapigano na maafisa wa serikali wakiondoka wakati ambapo waasi wamerejesha mikononi mwao enro kubwa la jimbo hilo.
Miezi minane ya mapigano kati ya waasi na majeshi ya serikali yamesababisha maelfu ya watu kuuawa huku zaidi ya watu milioni mbili wakiyakimbia makazi yao.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa (UN), watu 400,000 wanakabiliwa na baa la njaa,hasa katika eneo la kaskazini mwa jimbo hilo.
Waasi hao wa TPLF awali walieleza kwamba kusitisha huko wanakokusema majeshi ya serikali ni danganya toto na kwamba wataendelea kuwafurusha maadui zao hao kutoka katika eneo hilo.
Pamoja na hilo waasi hao wameongeza orodha mpya ya masharti ili waweza kusititisha mapigano, ikiwemo kufanyika kwa uchunguzi huru kuhusu madai ya uhalifi wa kivita, kupelekwa kwa misaada ya kibinadamu na kurejeshwa kwa huduma muhimu kama umeme.
Mpaka sasa serikali ya waziri mkuu Abiy Ahmed mjini Addis Ababa imekataa kuzungumza na kukubaliana na viongozi wa TPLF na kuliweka kundi hilo kama miongoni mwa makundi ya kigaidi.

No comments:
Post a Comment