Mahakama ya Katiba ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo imemuachia huru Waziri Mkuu wa zamani Augustin Matata Ponyo baada ya kubadili uamuzi wake wa kumuweka katika kizuizi cha nyumbani.
Wakili wa Matata, Laurent Onyemba amesema mteja wake hayuko tena kwenye kizuizi cha nyumbani na amerejea nyumbani kwake bila ya kusindikizwa na polisi.
Uamuzi wa mahakama hiyo umetolewa siku moja baada ya kumuweka Matata katika kizuizi cha nyumbani wakati akisubiri uchunguzi wa madai ya ubadhirifu wa fedha za umma yanayomkabili.
Jaji wa mahakama hiyo amesema Matata hawezi kukimbia na anaweza kuitikia mialiko ya upande wa mashtaka kama mtu huru.
Mwezi Mei, waendesha mashtaka walilitaka Bunge la Kongo kumuondolea Matata ambaye ni seneta kinga ya kutoshtakiwa, ili aweze kuchunguzwa kwa madai ya ufisadi yanayomkabili. Hata hivyo, Matata amekuwa akikanusha madai hayo.

No comments:
Post a Comment