Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatarajia kukutana wiki ijayo kuujadili mgogoro kati ya Sudan, Ethiopia na Misri uliosababishwa na mradi mkubwa wa bwawa la umeme uliojengwa na Ethiopia. Balozi wa Ufaransa kwenye Umoja wa Mataifa Nicolas de Riviere ametoa taarifa hiyo.
Mapema mwezi uliopita nchi za kiarabu zilitoa wito kwa Baraza la Usalama kuujadili mgogoro huo na mpango wa Ethiopia wa kujaza maji kwenye bwawa hilo kwa mara ya pili bila ya makubaliano na Sudan na Misri.
Hata hivyo Ethiopia haipendelei mradi huo uliopo kwenye mto wa Blue Nile ujadiliwe kwenye Umoja wa Mataifa. Badala yake inataka swala hilo lishughulikiwe kwenye Umoja wa Afrika.
Hapo awali Ethiopia ilipinga miito juu ya kuhusishwa kwa wapatanishi kutoka nje ya bara la Afrika. Balozi wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa De Riviere ambaye ni rais wa baraza la usalama mwezi huu wa Julai amesema hakuna zaidi ambacho baraza hilo linaweza kukifanya licha ya kuwaleta pamoja wahusika wote ili waeleze misimamo yao na kuwahimiza kurejea kwenye meza ya mazungumzo.

No comments:
Post a Comment