Mwekezaji bilionea na mshauri wa zamani wa Donald Trump Thomas Barrack amekana mashtaka ya kuwa ajenti wa serikali ya kigeni.
Bwana Barrack, 74, alikuwa msaidizi muhimu kwa Bwana Trump wakati wa kampeni yake mnamo mwaka 2016.
Ameshtumiwa kwa kushawishi kinyume cha sheria kwa niaba ya Nchi ya Falme za Kiarabu (UAE) wakati na baada ya uchaguzi, pamoja na kusema uwongo kwa FBI.
Bwana Barrack alikanusha madai hayo wakati akiwa mahakamani kwa mara ya kwanza Jumatatu.
Afisa huyo wa zamani wa Trump anakabiliwa na mashtaka ya kula njama, kuzuia haki na kutoa taarifa nyingi za uwongo kwa FBI wakati wa mahojiano ya 2019 na alikamatwa huko California wiki iliyopita.
Alipoondoka mahakamani Jumatatu, Bwana Barrack aliwaambia waandishi wa habari kuwa: "Kama munavyotarajia, mfumo unafanya kazi ... nyote mtaona kuwa sina hatia kwa asilimia 100".
Mfanyakazi wa Bw. Barrack, Matthew Grimes, pia anakabiliwa na mashtaka ya ushawishi haramu na alikanusha madai dhidi yake Jumatatu.
Raia wa UAE, Rashid Sultan Rashid Al Malik Alshahhi, 43, pia alishtakiwa ingawa bado hajakamatwa.
Wanaume hao watatu wanashutumiwa kwa kujaribu kinyume cha sheria kukuza masilahi ya serikali ya UAE kwa kutumia uhusiano wa Bwana Barrack kushawishi maafisa na kuonekana kwenye vyombo vya habari.
Pia inadaiwa walipigia debe kugombea kwa mtu anayependelewa na UAE kama balozi wa Marekani huko Abu Dhabi.
Bwana Barrack, ambaye pia aliwahi kuwa mwenyekiti wa kamati ya uzinduzi ya Bw. Trump, alikuwa marafiki na rais huyo wa zamani kwa miongo minne.
Mwekezaji huyo tajiri ndiye msaidizi wa zamani wa Trump kukabiliwa na mashtaka ya jinai hivi karibuni kama mwenyekiti wa zamani wa kampeni Paul Manafort na wakili wa zamani wa Shirika la Trump Michael Cohen.
Anatarajiwa kufika tena mahakamani Septemba 2.
Bwana Barrack kwa sasa ameachiwa kwa dhamana ya $ 250m (£ 180m), lakini lazima avae bangili ya kiwiko yenye GPS ya elektroniki, ambako kunamzuia kufanya safari na pia afuate amri ya kutotoka nje.

No comments:
Post a Comment