Mawakili wa kiongozi wa kundi lililopigwa marufuku na ambalo linataka kujitenga kwa jimbo la kusini -mashariki mwa Nigeria, Nnamdi Kanu wamesema kuwa wamenza kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Nigeria na Kenya kwenye Tume ya haki za binadamu ya Umoja wa Afrika.
Wanadai kuwajibika kwa nchi hizo mbili kwa madai ya kutofuata taratibu zinazopaswa za kumrudisha mteja wao.
Mwanasheria wa Bw. Kanu, Alloy Ejimako amesema kwenye taarifa yao kuwa suala hilo wamelifikisha Umoja wa Afrika kwa kuwa Nigeria na Kenya ni wanachama wa mkataba unaounda tume ya AU ya haki za binadamu.
Wanasheria wa Kanu wanaomba Kanu apelekwe Kenya kama mtu huru na raia wa Uingereza, wakidai kuwa kukamatwa kwake ni batili kwa kuwa taratibu hazikufuatwa katika kumrudisha nchini Nigeria.
Bw. Kanu ana uraia wa Uingereza na mazingira ya kurudishwa nchini Nigeria mwezi uliopita hayajulikani. Serikali ya Kenya ilikana madai ya kumkamata na kumrudisha Nigeria.
Hatua hiyo ilikuja baada ya serikali ya Nigeria kushindwa kumfikisha Bw. Kanu mahakamani kuendelea na mashtaka dhidi yake ya uhaini na mashtaka yanayohusiana na ugaidi.
Mahakama ya juu jijini Abuja imeiamuru mamlaka kumfikisha mahakamani tarehe 21 mwezi Oktoba.

No comments:
Post a Comment