Search This Blog

Monday, May 10, 2021

Serikali ya Umoja wa kitaifa Zanzibar(SUK) yafanikiwa kuwaunganisha wazanzibar pamoja na kuchangia maendeleo ya nchi


Na Thabit Madai,Zanzibar.                                                            

NI ukweli usiopingika ya kuwa  katika harakati za kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu huambatana na mambo mengi yakiwemo rushwa, vitisho, kuchafuliana majina kwa lengo la kushushiana hadhi.

Wagombea katika majimbo mbali mbali nchini huamua kufanya vitendo hivyo kwa lengo la kila mmoja kuweza kujinyakulia ushindi kama ilivyozoweleka kutamkwa kwamba ushindi wa kishindo.

Hali hii inaleta wasi wasi juu uwezekano wa kuvunjika kwa hali ya utulivu na Amani katika nchi, jambo ambalo halipendelewi na walio wengi kuona Nchi inaingia katika mifarakano inayosababishwa na utofauti wa itikadi za vyama cha kisiasa.

Uzoefu wa nchi yetu katika kipindi cha Uchaguzi Mkuu ndicho kipindi kinachoteka hisia za watu wengi huku kukiripotiwa matukio mbalimbali ya uvunjifu wa haki za binadamu pamoja na hali ya  Amani na usalama.

Ikumbukwe kuwa, hadi sasa Zanzibar imepitia chaguzi kuu sita (6) tokea Tanzania kuingia katika mfumo wa vyama vingi, ambapo vipindi hivyo vilikuwa vya chungu na moto, Jamii ilifarakana kwa kiasi kikubwa, watu walikuwa wanaishi bia ya maelewano wala masikilizano kutokana kutofautiana vyama vya Siasa.

Ilifikia wakati watu ndani ya visiwa hivi walikuwa wakiishi bila ya kusaidiana, waliishi kwa chuki na uhasama wa hali ya juu  kutokana na utofauti wa vyama vya kiasa, wakati huo huo matukuio mbalimbali ya ukiukwaji wa haki za binadamu yalikuwa yanaripotiwa kila mara.

Hali hiyo imegeuka  ilipofika Uchaguzi wa Mwaka 2020  mambo hayauwa kama yalivyozoeleka kuwa kabla,wakati, na hata baada ya uchaguzi mkuu ambapo hali ilikuwa ya Usalama, Amani na tulivu na bila ya kuripotiwa hovyo matukio ya uvunjifu wa haki za binadamu na usalama wa raia.

‘Nyota njema huonekana Asubuhi’, Baada ya kipindi cha Uchaguzi Mkuu kupita  Jamii bado iliendelea kuishi kwa Amani tena kwa umoja ambao uliunganishwa na vyama vikuu vya siasa Chama cha Mapinduzi CCM na Chama cha ACT  Wazalendo pale vilipoamua kushirikiana na kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa jambo ambalo si geni kushuhudiwa visiwani Humu.

Uwamuzi huo ulitokana pale tu  Rais Mwinyi alipoingia rasmi madarakani Novemba 02 na kuchukua uwamuzi wa kuwaandikia barua chama cha ACT Wazalendo kujiunga katika Serikali ya pamoja ya Umoja wa Kitaifa (SUK).

Decemba 06, 2020 Chama cha ACT Wazalendo kilikubali kuingia katika Serikali ya Umoja wa kitaifa ambapo ilipofika Decemba 08, 2020 Marehemu Maalim Seif sharif Hamadi aliapishwa kuwa Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar.

Mwanzo mpya wa Wazanzibar hapo ulishuhudiwa watu walifurahi kwa pamoja huku Dufu na ngoma mbalimbali zilipigwa yote kuonesha furaha yao ya kuwa pamoja kama ilivyokuwa mwaka 2010.

Vyama vya Siasa, Wanaharakati pamoja na jamii kwa ujumla haikuwa mbali imetoa neno kuhusu mafanikio yaliyopatikana mara baada ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa kitaifa (SUK).

VYAMA VYA SIASA VYAELEZA MAFANIKIO YA SUK

ACT WAZALENDO

KATIBU wa Itikadi, Uwenezi na Mawasiliano Taifa chama cha ACT- Wazalendo Salim Bimani alieleza chama cha ACT Wazalendo wanaridhishwa na muenendo mzima  wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ukizingatia wao ni moja ya sehemu ya Serikali hiyo.

Alisema kuwa Serikali iliamua kwa makusudi kungia katika SUK, imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuwaunganisha watu wa Zanzibar bila ya kujali vyama vyao vya kisiasa, sehemu wanapotokea na hata dini walizokuwa nazo.

Aidha alisema hakuwahi kuona wakati bora kama wakati wa Dk Hussein Ali mwinyi ambapo jamii inaishi kwa kupendana, kusaidiana bila ya kujali tofauti zao walizokuwa nazo hapo awali.

“Ukweli kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Dk Hussein ali Mwinyi ambayo ni serikali ya umoja wa kitaifa imefanikiwa kuwaunganisha watu pamoja bila ya kujali tofauti zao kisiasa,” alieleza Bimani.

Bimani alieleza kuwa Dk. Mwinyi alionekana tangu kipindi cha kampeni ambapo alikuwa na dhamira ya kuongoza Zanzibar kwa misingi yote ya haki za binadamu huku akiwa na dhamira ya kuwunganisha wazanzibar pamoja.

Aliongeza kuwa chama cha ACT Wazalendo hakitakuwa nyuma katika kuunga mkono jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali ya awamu ya Nane katika kuwahudumia watu wake.

Bimani alieleza  utendaji kazi wa Rais Dk Mwinyi na Serikali ya Umoja wa kitaifa na kusema kwamba, Dk. Hussein Ali Mwinyi amekuwa akifanya kazi nje ya mfumo wa Chama cha Mapinduzi CCM aliodai kuwa mfumo huo ulikuwa wa kulinda.

Hata hivyo Bimani alisema kuwa, Muelekeo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuweka aman na umoja na utulivu kwa Wazanzibar wote ukizingatia nchi imetoka katika uchaguzi mkuu ambapo watu waligawika kutokana na vyama vyao.

“Ukweli kuwa  Serikali ya Umoja wa kitaifa na uongozi wake Dk Hussein Mwinyi nchi imekuwa katika hali ya Amani na utulivu kwa Wanzanzibar wote pamoja na kutoripotiwa kwa matukio ya uvunjifu wa haki za binadamu,” alisema.

Alifafanua kuwa  Uongozi wa Dk Mwinyi   mashirikiano baina ya jamii na Serikali yameongezeka kutokana kuwa wananchi wanahubiriwa umoja na Amani pamoja mashirikiano baina yao.

“Uongozi wa Dk Hussein Ali Mwinyi umeanza kuleta  mwanga mpya katika jamii ambapo Serikai yake anayoongoza imepunguza chuki kwa wanzanzibar hasa msimamo wake aliouonesha tangu awali alipoapishwa na kutoa mkono wa mashirikiano ambapo amekuwa akihubri amani, umoja na mashirikiano,” alieleza Saum Bimani.

 Salumu Bimani hakuacha kutaja mafanikio yaliyopatikana na Serikali ya Mapinduzi ya kwa kipindi kifupi tangu kuingia madarakani, alisema imefanikiwa kurejesha Imani ya wananchi na kufanikiwa kujipambanua kuwa inahitaji maendeeo ya haraka kwa wazanzibar wote.

“Mimi nataka niseme kwamba sisi kama chama cha ACT Wazalendo tumeona kuwa uongozi wa Dk Hussein Ali Mwinyi ni uongozi wa mfano wake kutokana kuwa kwa kipindi kifupi tayar tumeshaanza kuona neema na mafanikio kadhaa hivyo kwetu sisi tutaendelea kumuunga mkono kwa hali na mali,” alieleza Salum Bimani.

DEMOKRASIA MAKINI (DM)

Katibu Mkuu wa chama cha Demokrasia Makini,  Ameir Hassan alisema kwamba uwepo wa Serikali ya Umoja wa kitaifa ni ishara tosha ya uongozi uliotukuka wa Dk Hussein mwinyi ambapo ameonesha kuwa serikali yake imedhamiria kwa vitendo ujenzi wa Zanzibar mpya.

Alisema kwamba kwa muda mrefu sana Wazanzibar walikuwa na shauku ya kuona ujenzi wa Zanzibar mpya ambayo haitakuwa inabaguwa watu katika imani zao na hata  vyama vyao vya Siasa ambapo muelekeo huo umeonekana kwa Dk Hussein Mwinyi na Serikali ya kitaifa.

“Ni jambo lililokuwa wazi ndani ya uongozi wa Dk.Hussein Ali Mwinyi amefungua macho wazanzibar kwa kuwaonesha muelekeo wa Serikali yao, pamoja na kuwashirikisha kwa pamoja bila ya kujali vyama vyao,” alisema Ameir.

 UPDP

Hamadi Ibrahimu ni katibu Mkuu wa Chama UPDP alisema kuwa kwa kiasi kikubwa anaridhishwa na muenendo wa Serikali ambayo imehusisha vyama pinzani katika uundaji wa Serikali hiyo.

Alisema kuwa kwa muda mfupi Serikali imejitengenezea uwaminifu kwa wananchi wake kutokana na kuwa Serikali yao ina watu wa vyama tofauti.

“Hata hivyo kitendo cha Rais, Makamu wa kwanza wa Rais na Makamu wa Pili wa Rais kutumia misikiti kwa kuhubiri amani na ujenzi wa Zanzibar mpya ni moja nyenzo ilitengenezwa ya kuwaunganisha watu na kujeng Imani na Serikali yao,”alieleza.

Katibu Mkuu huyo hakuacha kumuelezea utendaji kazi wa  Dk Mwinyi na kusema kwamba naona kasi aliyoanza nayo Rais Dk Hussein Ali Mwinyi si nguvu ya soda kama inavyodhaniwa na baadhi ya watu.

Ibrahimu  alisema hata alipokuwa waziri wa ulinzi na mbunge wa Kwahani , Dk Mwinyi  alikuwa akifanya kazi kwa kasi na umakini mkubwa.

Alisema anachopaswa kuendelea kukifanya Dk Hussein Mwinyi na Serikali yake   ni kuwadhibiti watendaji wasio na maadili na kuweka mfumo mzuri wa utendaji kazi kwa viongozi wote kuanzia ngazi ya chini.

“Serikali inatakiwa kuweka mfumo wenye watendaji waadilifu watakaofanya kazi kwa kasi kama ya Rais ili tuweze kuyafikia mafanikio.

“Tunajua kuwa Rais hawezi kusimamia kila mahali, bali akiwa na watendaji waaminifu, mambo yatakwenda kama anavyotaka iwe,” alisema.

CHAMA CHA MAPINDUZI CCM

Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Ueneze CCM Zanzibar, Catherine Peter nao yeye amefika mbali zaidi katika kueleza mafanikio ya Serikali ya umoja wa kitaifa na kueleza kwamba Nchi ipo salama kutokana kuwa kiongozi wa Nchi ameonesha wazi kutaka umoja, maendeleo na kuinua uchumi imara wa Zanzibar.

Aliongeza kuwa, hana mashaka na viongozi waliopo sasa anajua wanayo dhamira ya kweli ya kuitumika nchi hii sambamba na kuendelea  kuwa na mshikamano wa pamoja.

WANANCHI

Fatma Abdallah (34) mkaazi wa mtoni Daraja bovu anaeleza kuwa uwepo wa Serikali ya umoja wa kitaifa umeweza kuwaunganisha watu pamoja na kupelekea Serikali kuwahudumia wananchi katika maeneo yao bila ya kujali vyama vya siasa na sehemu wanayotokea.

“Ukweli usemwe hapo nyuma watu tunaishi huku ilionekana kuwa ni wapinzani baadhi ya huduma muhimu tulikuwa hatupatiwi na Serikali ila kwa sasa tunashukuru serikali hii imekuja kutuunganisha pamoja,” alieleza.

Nae Bi Asha Abdallah shauri (60) Mkazi wa Mikunguni Unguja, alieleza kuwa ameshuhudia uwepo wa awamu kadhaa za Serikali zilizopita ila uongozi wa awamu ya Nane anauwona ni wa tofauti kwani wananchi wanaishi kwa furaha bila ya chuki.

“Mwanangu nmeshuhudia Viongozi mbalimbali wakiongoza hapa kwetu, mambo hayakuwa hivi, kipindi kama hichi tumetoka katika uchaguzi ungekuwa unasikia kila siku unasikia watu wamechoma mikarafuuu, watu wamepigwa, watu wanatafutwa ila sasa hatujasikiapo chochote kutokea,” alieleza.

“Mungu amajaalie huyu kijana wetu aendelee na moyo wake mzuri wa kuwaunganisha watu pamoja bila ya kujali tofauti zao,” aliongeza Bi Asha Abdallah.

“Bila shaka ndugu mwandishi ulikuwepo katika viwanja vya maisara wakti wa Sherehe za mapinduzi za mwaka huu, uliona wakati wa mazishi ya Maalim Seif, ulishuhudia wakati wa kuagwa kwa Dk. Magufuli, hii ndio Zanzibar tuliokuwa nayo miaka iliyopita tupo wamoja tunaishi kwa kupenda tena kwa misingi ya Dini zet,”alianza kwa kueleza Mohamed Abdallah (42) Mkaazi wa Mikunguni.

Alieleza kuwa anapoulizwa mafanikio ya umoja wa kitaifa SUK, hasiti kutaja matukio hayo ambayo anaokuwa ni mafanikio mkubwa watu wanajumuika pamoja katika mambo ya msingi.

“Hapo awali hatukuwa hivyo kiongozi wa upinzani afariki chama kingine kijitokeze kwa wingi tena kwa huzuni ule, ukweli kuwa sasa Zanzibar tupo wamoja kutokana na uwepo wa Serikali ya Umoja wa kitaifa,”aliongeza kueleza.

Kwa upande wake Zahran khamisi (46) alisema Uongozi wa Dk Mwinyi umekuwa uongozi makini ukilinganisha uongozi uliopita kutokana kuwa kwa muda mrefu wazanzibar walitamani kuishi pamoja bila ya tofauti za kisiasa.

“Tulikuwa katika ambacho watu tunaishi kwa kuangaliana machoni,tulitamani kuishi kama tunavyoishi hivi ila hatukupata kiongozi wa kuweza kutuunganisha pamoja,” alisema.

“Mwandishi ukitaka kujua kama serikali hii ipo makini angalia kipindi ambacho maalim Seif amefariki watu wengi tulidhani labda ndio mwisho wa Serikali ya kitaifa, ila hapana bado Serikali ilikuwa dhamira na akapatikana kiongozi mwingine jahazi bado linaendelea,” alieleza.

RAIS DK HUSSEIN ALI MWINYI

Kwa nyakati tofauti tofauti Dk. Hussein Ali Mmwinyi amekuwa akieleza kwamba, Serikali ya Umoja wa Kitaifa imedhamiria kuendeleza amani, umoja na mshikamano kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wa Zanzibar.

Dk.Mwinyi alisema kuwa  kuwepo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa imeweza kuimarisha amani, umoja na mshikamano hapa Zanzibar hatua ambayo ni chachu ya maendeleo na imekuwa ikisisitizwa siku zote na waasisi wa taifa hili.

 Hata hivyo Dk.Mwinyi ametaja mafanikio ya uwepo wa Serikali ya Umoja wa kitaifa, amesema kuwa hadi  hivi sasa kumekuwepo maelewano na mashirikiano makubwa kati ya viongozi pamoja na wananchi walio wengi wa Zanzibar hali ambayo imepelekea kuimarika kwa umoja, amani na mshikamano tokea kumalizika kwa uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 hapa nchini.

Aliongeza kuwa hatua hiyo imefikiwa kutokana na maridhiano yaliyofanyika ikiwa ni pamoja na kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo lengo na madhumuni yake makubwa ni kuendeleza umoja, amani na mshikamano ili Zanzibar izidi kupata maendeleo na wananchi wake wazidi kuelewana.

 



No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...