Na Omary Mngindo, Chalinze.
MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imewaasa wakazi wa Kijiji cha Mazizi Kata ya Msata kuacha kutumia maji yaliyomo katika mabwawa kwani si salama kwa afya zao.
Kijiji cha Mazizi ni mojawapo ya vijiji vinavyonufaika na mradi wa maji kipitia Mamlaka hiyo, ambapo sasa wananchi wanapata maji safi na salama kutoka kwenye mtambo wa kuzalisha maji wa Wami uliopo Kata ya Msata.
Akitoa elimu kwa viongozi wa vitongoji vya Kijiji cha Mazizi, Afisa Maendeleo Jamii wa DAWASA Elizabeth Eusebius amesikitishwa kuona wanakijiji bado wanatumia maji ya visima ambayo si salama kwa kupikia na kunywa hasa kipindi cha mvua.
"Matumizi ya maji machafu husababisha magonjwa ya tumbo, kuhara na kuleta athari kwenye ukuaji wa mtoto, niwaombe viongozi tuendelee kuwapatia elimi wananchi wetu watumie maii safi na salama yanayoletwa kwetu na Serikali yetu," alisema Eusebius.
Eusebius ameongeza kuwa matumizi ya maji machafu ni hatari kwa afya ya binadamu, na ndio maana serikali inajitahidi kuwekeza fedha nyingi katika kutekeleza miradi mikubwa ya kusambaza maji kwa wananchi wote.
"Serikali inatumia gharama kubwa kujenga miradi mikubwa ya kusambaza maji kwa wananchi ili watumie maji masafi na kuepuka matumizi ya maji machafu," alisema Eusebius.
"Maji yanayozalishwa na mtambo wa DAWASA Wami ni maji masafi yanayofaa kutumika kwa matumizi ya nyumbani na kwenye shughuli mbalimbali za kiuchumi," amesisitiza.
Aidha amewasisitizia kuhusu umuhimu wa kuweka na kutunza Mazingira safi ikiwa ni pamoja na kulinda vyanzo vya kuzalisha maji ili huduma ya maji iwe endelevu.
"Usafi ni afya, na kila mtu akijali usafi na kuweka Mazingira safi tutaweza kuboresha afya na kuwa mbali na magonjwa," amesema.
Ameeleza kuwa ni wajibu wa viongozi wa vitongoji kuwaelimisha wananchi kuacha kutumia maji machafu na kutumia maji masafi ya bomba, ambayo serikali inaendelea na juhudi za uboreshaji.
Pia amewataka viongozi hao kua karibu na ofisi ya DAWASA Mkoa wa Chalinze ili kupata taarifa, ufafanuzi wa miradi ya maji inayoendelea kutekelezwa na katika jimbo la Chalinze, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vituo vya maji katika vitongoji ambavyo havijafikiwa na huduma hiyo.
"Tunaendelea na juhudi za kuhakikisha kuwa maeneo yote yanakuwa na maji kupitia mradi wa awamu ya kwanza na pili, ili kujifunza kuhusu kazi zinazofanywa na Mamlaka katika eneo lao ili waweze kuwaelimisha wananchi.
Mbali na hayo, Bi Eusebius amewataka viongozi na wananchi kwa ujumla kuwasiliana na ofisi ya DAWASA Mkoa wa Chalinze kupitia namba za huduma kwa wateja ambazo ni 0752 801 178 na 0800 110 064.


No comments:
Post a Comment