Na Ahmad Mmow, Lindi.
Katika kuinua kiwango cha uzalishaji wa korosho na ufuta wilayani Nachingwea, halmashauri ya wilaya hiyo iliyopo mkoani Lindi imezalisha miche 1,558,000 ya mikorosho.
Hayo yalielezwa jana mjini Lindi, na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Hassan Rugwa kwenye mkutano maalumu wa wadau wa ufuta na korosho katika mkoa wa Lindi.
Rugwa alisema ili kuongeza kiwango cha uzalishaji wa korosho, halmashauri ya wilaya hiyo imezalisha 1,558,000 miche ya zao hilo kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2015 hadi 2021. Miche ambayo imezalishwa katika ekari 63,000.
Alisema kuanzia mwaka 2015 hadi 2020 halmashauri hiyo ilizalisha miche 1,538,000 kwenye ekari 61,520. Ambapo mwaka huu (2021) imezalisha miche 37,000 iliyopo katika ekari 1,480.
Alisema mwaka huu halmashauri hiyo imetenga na kupanga kutumia shilingi 10,000,000 kwa ajili ya kuzalisha na kusambaza miche 20,000 kwa wakulima.
'' Miche 17,000 kati ya 37,000 iliyozalishwa mwaka huu imezalishwa na wakulima. Miche 20,000,000 ambayo itasambazwa na halmashauri imezalishwa na halmashauri yenyewe,'' alisema Rugwa.
Mbali na miche ya mikorosho, mkurugenzi huyo alisema mwaka huu halmashauri hiyo imelima ekari 25 za ufuta katika kijiji cha Rweje, kata ya Mkoka. Huku akibainisha kwamba dhamira ni kulima ekari 100. Ambapo matarajio ni kuvuna kilo 10,000 ambazo ni kwa ajili ya mbegu.
'' Katika kata 21 kati ya 36 zilizopo katika halmashauri ya wilaya ya Nachingwea kuna mashamba darasa 42. Kila kata ina ekari mbili na kwenye kata 15 ekari moja kila kata, kwahiyo tuna ekari 57 sawa na matarajio ya kuvuna kilo 22,800 za mbegu,'' Rugwa alibainisha.
Aidha Rugwa alitaja kiasi cha fedha kinachotengwa kwenye bajeti kuwa ni shilingi 50,000,000 kwa muda wa miaka mitano ili kufikia lengo la kulima ekari 20,000 za mikorosho.
Kwa upande wa ufuta, Rugwa alisema halmashauri hiyo inatenga shilingi 20,000,000 kila mwaka kwa ajili ya zao hilo kwa kipindi cha miaka mitano sawa na ekari 4000 kila mwaka ambazo zitafanya kuwa najumla ya ekari 20,000 katika kipindi hicho cha miaka mitano.

No comments:
Post a Comment