Na John Walter-Babati
Wananchi wametakiwa kutambua kuwa jukumu la kutunza na kuvilinda vyanzo vya maji linamhusu kila mmoja na sio kuiachia serikali pekee.
Hayo yameelezwa na Katibu Tawala Rasilimali mkoa wa Manyara Dominick Mbwete wakati akizindua Jumuiya za Watumiaji Maji bonde dogo la Kiru-Magugu, Kisangaji-Magara hafla iliyofanyika katika Hotel ya White Rose Mjini Babati.
Jumuiya hizo zimeundwa na Bodi ya Maji Bonde la Kati kwa kushirikiana na viongozi wa vijiji na kata ambao ni wawakilishi wa wananchi wanaotumia mabonde hayo kwa ajili ya kuhifadhi vyanzo vya maji mkoani Manyara.
Ameitaka jamii kuzingatia utunzaji wa Mazingira na uhifadhi kwa kuwa madhara ya uharibifu ni makubwa na huwa hayaonekani kwa haraka na ni vigumu kuyarudisha katika hali yake ya kawaida.
Mbwete amezitaka jumuiya hizo zikasimamie kikamilifu shughuli zao kwa kuzingatia miongozo kutoka kwenye katiba ambayo wameitengeneza.
Pamoja na hayo, alizikabidhi jumuiya hizo vitendea kazi zikiwemo piki piki na katiba ambayo itawaongoza katika kutimiza majukumu yao.
Kaimu mkurugenzi Bonde la Kati Elibariki Shanguya amesema Serikali kupitia Wizara ya Maji iliamua kuunda Jumuiya hizo za maji ili kukabiliana na tatizo la upungufu wa rasilimali za maji.
Alisema Jumuiya hizo ndio msingi, hivyo zikiboreshwa na kuimarika kwa kupata ushirikiano katika vijiji hali ya vyanzo vya maji itakuwa salama.
Akizungumza kuhusu uanzishwaji wa jumuiya hiyo Afisa Maendeleo ya Jamii Mwandamizi wa Bodi ya Maji Bonde la Kati, Nelea Bundala alisema jumuiya hiyo itasaidia kulinda vyanzo vya maji ambavyo vinaharibiwa kutokana na shughuli mbalimbali za kibinadamu zikiwemo za kilimo zinazofanywa pembezoni mwa Vyanzo hivyo.
Alisema kwa kuwa wao kazi yao kubwa ni kusimamia rasilimali za maji ili ziwe endelevu kwa vizazi vilivyopo na vijavyo wameona ni muhimu kuwepo na jumuiya ya watumia maji hususani katika Mabonde hayo muhimu ili kuhakikisha yanadumu na wanayatumia kwa mujibu wa sheria zilizopo.
Bundala alisema sheria inaelekeza kwamba mtumiaji wa maji ndiye mtunzaji namba moja wa maji kwa sababu ni mnufaika na yupo maeneo ya vyanzo vya maji husika.
Alisema walivitembelea vijiji vyote vilivyopo katika jumuiya hizo na kufanya mikutano ambapo walitoa elimu namna ya kusimamia taratibu za kuvilinda vyanzo vya maji huku wawakilishi wakiwa ni kutoka kundi la wafugaji, wakulima na watumiaji wa maji .
Alisema mchakato huo umewamewashirikisha viongozi wa vijiji kwa sababu wao ni walinzi wa amani, wasimamizi wa kuu ngazi za vijiji hivyo jumuiya haiwezi kufanya kazi peke yake bila ya kushirikiana na vijiji.
Alisema lengo ni kuhakikisha kama wizara ya maji wadau wanaielewa sera , sheria na kuunda vyama vya watumia maji viweze kuhakisha vinafanya kazi kwa niaba ya bonde kusaidia wizara kutunza mazingira na vyanzo vya maji.
Wakizungumzia jumuiya hizo Mwenyekiti wa Jumuiya ya Bonde dogo la Kiru-Magugu Mathayo Molel, Mtendaji kata ya Magara Beatrice Fernandez na madiwani kutoka katika kata za Kiru,Magara, Magugu na Kisangaji wameiopongeza serikali kwa jitihada hizo na kuahidi kuhimiza jamii kulinda na kuheshimu vyanzo vya maji.
No comments:
Post a Comment