Mataifa ya Ulaya yanataka majibu baada ya maafisa wa Belarus kuitumia ndege ya kivita kuilazimu ndege moja ya abiria kuubadili mkondo na kuelekea mji mkuu Minsk, ambapo mwanahabari mkosoaji aliyekuwemo alikamatwa.
Shirika la ndege la Ryanair limesema ndege yake ilikuwa safarini kutoka Ugiriki kuelekea Lithuania jana wakati ilifahamishwa kuhusu kitisho cha usalama na waongozaji wa safari za ndege nchini Belarus na kuwambiwa waipeleke Minsk ili kutua kwa dharura.
Ndege hiyo ilitua salama na hakuna bomu lililopatikana baada ya upekuzi. Lakini maafisa walitumia fursa hiyo kumkamata Raman Protasevich, mwanahabari na mwanaharakati wa upinzani Belarus, ambaye alikuwa miongoni mwa abiria.
Serikali za Ulaya zimezungumza kwa hasira, zikisema Rais wa kiimla wa Belarus Alexander Lukashenko alitumia kisingizio cha kitisho cha usalama ili kufanya utekaji nyara wa ndege ya abiria ili kumkamata mkosoaji wa serikali. Ndege hiyo ilikuwa na abiria 123.

No comments:
Post a Comment