Search This Blog

Wednesday, April 14, 2021

Mgombea urais TLS aahidi kufuta sheria kandamizi bungeni



 Mgombea urais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Flaviana Charles amesema akichaguliwa atashirikiana na Bunge kurekebisha sheria kandamizi.

Flaviana aliyasema hayo juzi jijini Dar es Salaam wakati wa mahojiano maalumu na gazeti hili akiwa mmoja kati ya wagombea watano waliojitokeza kuwania nafasi hiyo ya juu katika chama hicho cha kitaaluma nchini.

Flaviana ni mwanamke pekee aliyejitokeza kugombea nafasi hiyo katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Aprili 16. Wagombea wengine ni aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hosea pamoja mawakili maarufu nchini akiwamo lbert Msando, Shehzad Wall na Rais wa zamani wa chama hicho, Francis Stolla.

Flaviana alisema zipo sheria ambazo zimekuwa zikilalamikiwa, hivyo TLS kama chama chenye wajibu kwa jamii itahakikisha inahamasisha mabadiliko ya sheria hizo na kuimarisha utawala wa sheria nchini.

“Tutashirikiana na Bunge kuhakikisha sheria kandamizi zinafanyiwa mabadiliko. Tutafanya mchakato wa kuzipitia sheria hizo kwa kuwashirikisha wanasheria pamoja na wananchi kwa ujumla,” alisema Flaviana.

Wakili huyo ambaye pia ni mhadhiri wa Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema ataanzisha mkakati maalumu wa ushirikiano na Serikali, Bunge, Mahakama pamoja na wadau wengine wakiwamo wanaharakati na wananchi wa kawaida.

Alibainisha kwamba wanasheria wana wajibu kwa Mahakama, chama chao, jamii na wanataaluma wenzao kuhakikisha haki inatendeka. Hivyo, alisema atausimamia wajibu huo katika uongozi wake iwapo atapata ridhaa ya wanachama kuiongoza TLS.

“Tupo hapa kulisaidia Bunge, Serikali na Mahakama kuhakikisha haki inatendeka. Utungaji sheria ni mchakato, nasi kama wanasheria tuna nafasi ya kutoa maoni ili kuboresha sheria zetu,” alisema Flaviana ambaye aliwahi kuwa makamu wa rais wa TLS.

Kuhusu mabadiliko ndani ya TLS, Flaviana amesema amejipanga kuleta mabadiliko katika chama hicho ikiwamo kuzingatia maslahi ya makundi yote ya wananchi, wanasheria wachanga, wanawake na walemavu.

Alisema baadhi ya mipango yake endapo atachaguliwa ni kuunda kamati maalumu ya washauri ambayo itajumuisha majaji wastaafu, wanasheria wakongwe na viongozi wa zamani wa TLS, jambo litakalokifanya chama hicho kupiga hatua zaidi ya kuboresha hadhi ya wanasheria na kutoa huduma zaidi kwa wananchi.

Pia, alisema anakusudia kuanzisha vyanzo vingine vya mapato ili kuwapunguzia wanachama mzigo wa kukiendesha chama hicho. Alisema wanasheria wana uwezo mkubwa wa kuandika miradi au kuzungumza na wadau mbalimbali watakaokichangia chama kufanikisha mipango yake.

“Wanachama wetu wana kiu ya kujua mapato na matumizi ya fedha zao. Tutakuwa tunatoa ripoti na elimu endelevu kwa wanasheria na elimu hiyo itatolewa kwa bei ndogo ambayo haitawaumiza wanasheria wachanga hata wale wakongwe,” alisema.

Flaviana aliongeza kuwa atahakikisha anazungumza na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Profesa Adelardus Kilangi kili wanasheria wa Serikali nao warudi kuwa wanachama wa TLS tofauti na ilivyo hivi sasa.

“Siku hizi wanasheria wa Serikali wana chama chao, sasa tunatamani tuwe wamoja bila kujali huyu ni mwanasheria wa kujitegemea au wa Serikali. Nitamshawishi ndugu yangu Profesa Kilangi atafakari hilo,” alisema mwanamke huyo.

Flaviana ni mkurugenzi mtendaji wa shirika lisilo la kiserikali la Business and Human Rights Organization ambalo linashujighulisha na kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi kuhusu migogoro ya ardhi, mazingira, jinsia na kuhamasisha uwazi na uwajibikaji katika jamii hasa watendaji wa Serikali.

Mbali na hilo, yeye ni mhadhiri msaidizi katika Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako sasa anasomea shahada ya uzamivu (PhD). Alikuwa makamu mwenyekiti wa TLS mwaka 2016/17 na sasa ni katibu anayemaliza muda wake wa Chama cha Wanasheria Afrika.

Flaviana ni wakili wa kujitegemea ambaye moja ya kesi maarufu alizowahi kusimamia ni ile ya Watanzania waliokamatwa nchini Malawi kwa tuhuma za kufanya ujasusi. Alisimamia kesi hiyo mpaka Watanzania hao waliokuwa mahabusu kwa miezi sita wakashinda.



No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...