Mawaziri wa ulinzi na mambo ya kigeni wa Marekani na Ujerumani wamefanya mazungumzo kwa njia ya simu na kuahidi mwanzo mpya baada ya enzi ya Donald Trump iliyolemaza mahusiano kati ya Washington na Berlin.
Kwenye mazungumzo na mwenzake wa Ujerumani Annegret Kramp-Karrenbauer, waziri mpya wa ulinzi wa Marekani Lloyd Austin ameisifu Ujerumani kwa kuwa mwenyeji wa vikosi vya nchi yake na kuashiria kuwa atapitia upya uamuzi wa utawala uliopita wa kuondoa karibu theluthi ya wanajeshi wa Marekani nchini Ujerumani.
Uamuzi huo wa utawala wa Trump uliishangaza Ujerumani ambayo haikujumishwa kwenye majadiliano na ulitishia kuteteresha zaidi mahusiano baina ya mataifa hayo mawili wanachama wa Jumuiya ya NATO.
Kwa upande wake waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Heiko Maas aliyezungumza na mwenzake wa Marekani Antony Blinken wamekubaliana kufanya kazi pamoja katika masuala ya kuikabili China na uwezo wa nyuklia wa Iran.

No comments:
Post a Comment