HATIMAYE Kikongwe, Imbori Hando (72) mkazi wa Kibaya wilayani Kiteto mkoani Manyara, amerejeshewa eneo lake la ekari 27 alilokuwa ameporwa kwa miaka 10 iliyopita.
Makabidhiano ya eneo hilo yalifanyika Kijiji cha Ndaleta, chini ya Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Kiteto, Venance Sangawe aliyesimamia kupatikana haki hiyo.
Sangawe alisema walipokea lalamiko hilo na kulifanyia kazi na kubaini kuwa baadhi ya viongozi wa chama na Serikali walipotosha ukweli wa suala hilo kwa muda mrefu.
"Haikuwa rahisi Kikongwe huyu kupata haki yake..hata baadhi ya viongozi wa Serikali walichangia kuchelewesha haki ya mama huyu, kila tulipotaka kujua ukweli ulipindishwa"
Leo tumemkabidhi shamba lake ekari 27 mbele ya viongozi wa Kijiji Kata na Tarafa, baada ya kubaini ukweli wa jambo hili ambapo viongozi wengi Kiteto waliamua kuachana nalo.
Mama Imbori Hando, alishukuru Taasisi ya TAKUKURU Kiteto akisema, hakuna ofisi ambayo hakufika kulalamika, na kuambulia kuitwa kichaa ambaye alipuuzwa na viongozi hao.
"Nilipuuzwa kila kona, pamoja na kushinda kesi baraza la ardhi la kata na kukaza hukumu baadhi ya watumishi wa Serikali walishindwa kunisaidia huku nikidaiwa kuwa mimi nimechanganyikiwa kutaka kupotosha ukweli"
Takukuru Kiteto wameokoa shamba langu..hakika sina cha kuwalipa Mungu atawalipa, wenzangu waliyumbisha haki yangu kwa kutoa rushwa jambo ambalo limeharibu mfumo wa maisha yangu, alisema Mama Hando.
Kwa upande wake Joseph Kaaya mwangalizi wa haki za Binadamu Kiteto alisema pamoja na jitihada kubwa alizofanya kumwezesha kikongwe huyo kudai haki yake alicheleweshwa na baadhi ya viongozi wa vijiji na kata.
Alisema viongozi hao walidiriki kusimama hadharani kusema mama huyo anatatizo la akili kwa nia ovu kutaka kuharibu ushahidi akidai isingekuwa Taasisi ya TAKUKURU asingepata haki hiyo.
Maiko Baso mtoto wa kwanza wa mama huyo akizungumzia sakata hilo alisema, limechangia mama yao kuvunjwa mguu na baadhi ya maadui zake kwa kugongwa na pikipiki wakati akifuatilia haki yake hiyo.
Alisema kwa kipindi chote familia yao wamekuwa wakitishiwa maisha mbali na kuchomewa nyumba yao wakiwa huko shambani lakini kupatikana kwa haki hiyo kunaweza kurejesha imani na Serikali yao.

No comments:
Post a Comment