Na John Walter-Babati- Manyara
Katika kuendelea kudumisha mahusiano mema katika jamii,Taasisi ya Chechem inayohusika na uhifadhi wa wanyamapori katika wilaya ya Babati mkoani Manyara, imetoa msaada wa vitimwendo 30 (Wheelchair) kwa watu wenye Ulemavu wilayani humo.
Mkurugenzi wa Chemchem Nicolaus Negre amesema msaada walioutoa una thamani ya shilingi Milioni 21,000,000.
Negre amesema taasisi hiyo katika mwaka 2020 imefanikiwa kupata jumla ya baiskeli 242 nchi nzima kwa ajili ya kuwasaidia watu wenye ulemavu.
Mkuu wa mkoa wa Manyara Joseph Mkirikiti akizungumza wakati wa makabidhiano hayo aliwataka wananchi kuacha tabia ya kuwaficha watu wenye ulemavu na badala yake watoe taarifa ili waweze kupatiwa mahitaji muhimu.
Pamoja na hayo Mkirikiti ametoa msaada wa Mchele na fedha kwa watu wenye ulemavu ili waweze kufurahia siku kuu za mwisho wa mwaka.
Katibu wa Shirikisho la watu wenye ulemavu mkoa wa Manyara Mwalimu Peter Sanka, ameishukuru Taasisi ya Chem Chem kwa msaada huo na kusema kuwa Viti mwendo hivyo Vitawasaidia kwa sababu kabla ya kuvipata walikua wanashindwa kutembea kutoka sehemu moja hadi nyingine kufanya shughuli mbalimbali za uzalishaji mali.
Amesema wanafunzi wenye ulemavu waliofanikiwa kupata Vitimwendo hivyo vitawapunguzia majukumu wazazi waliokuwa wanatumia muda mwingi kuwapeleka shule ambapo kwa sasa wanafunzi wenzao wanaweza kutoa msaada kwa kusukuma kiti hicho wakati wa kwenda na kurudi shule huku wazazi wakiendelea na shughuli za utafutaji riziki za kila siku.
Afisa Ustawi wa Jamii wilaya ya Babati Mathias Fokasi amesema changomoto iliyopo kwa sasa kwa jamii ni kufichwa ndani watu wenye ulemavu jambo ambalo linapelekea kukosekana kwa taarifa sahihi na kudidimiza jitihada za kusaidia makundi hayo.
Amesema Halmashauri inatoa asilimia 2 kutoka vyanzo vya mapato ya ndani kwa ajili ya mikopo ya watu wenye Ulemavu ambapo mpaka sasa kuna vikundi 52 vilivyoundwa kwa ajili ya kupata mkopo huo, vikundi 46 vimekopeshwa shilingi milioni 74 hadi sasa.
Amesema halmashauri kwa kushirikiana na chama cha watu wenye ulemavu (SHIVAWATA) imewezesha kuwasafirisha kushiriki maazimisho yao ya kitaifa na makongamano mengine yanayofanyika ndani ya wilaya na mkoa.
Halmashauri ya wilaya ya Babati ina jumla ya Walemavu wapatao 1,811 ambapo kati yao wenye ulemavu wa viungo ni 249,magonjwa ya akili 546,wasioona 284,Bubu 288,wenye ualbino 10 na viziwi 222.
Hivi Karibuni Taasisi ya Chemchem ilikabidhi gari ya shule aina ya basi lenye thamani ya Zaidi ya shilingi Milioni 200 katika kijiji cha Mdori kata ya Nkaiti kwa ajili ya kuwapeleka na kuwarudisha nyumbani wanafunzi.

No comments:
Post a Comment