Search This Blog

Thursday, December 17, 2020

RC Mahenge aagiza kupatiwa ripoti ya madaraja yote yaliyosombwa na mvua



Na Ezekiel Mtonyole, Dodoma.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge amewaagiza Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Dodoma kupeleka taarifa ofisini kwake wakiainisha madaraja yote yaliyoharibiwa na mvua yaliyodumu kwa mda mfupi sambamba na wakandarasi waliotekeleza miradi hiyo.

Dkt Mahenge ametoa maagizo hayo Jijini Dodoma wakati wa kikao cha bodi ya mfuko wa barabara  Mkoa wa Dodoma ambapo amesema kumekuwa na tabia ya wakandarasi kujenga madaraja chini ya kiwango na kusababisha madaraja hayo kusombwa na maji kwa mda mfupi.

"Nataka nipate taarifa za Wakuu wa Wilaya zote maeneo gani madaraja yamevunjika na wakandarasi waliojenga miradi hiyo pia na wasanifu wa miradi hiyo haiwezekani tutumie fedha nyingi halafu mda mfupi madaraja hayo yasombwe na maji" amesema Dkt Mahenge.

Sambamba na hilo amewataka viongozi wa Wilaya na Halmashauri zote za Mkoa huo kujenga utaratibu wa kutembelea mara kwa mara miradi inayotekelezwa katika maeneo yao ili kuepuka ujenzi wa chini ya kiwango na miradi hewa kwenye maeneo yao.

Aidha ameziagiza taasisi za TANROADS, TARURA, TANESCO, RUWASA na Jiji la Dodoma kuandaa mipango mahususi ya namna bora ya kutekeleza miradi yao ya kutoa huduma za kijamii kwa wananchi ili kusiwepo na malalamiko ya mara kwa mara.

"Nataka muandae muongozo ambao unabainisha ni kwa namna gani wananchi watapata huduma kikamilifu katika maeneo yote, na TANROADS, TARURA na Jiji mhakikishe maeneo yote yanayohitaji taa yanawekewa haraka" amesema.

Amezitaka taasisi hizo kushirikiana katika kutoa huduma kwa wananchi na sio kila taasisi kufanya kazi kivyake na kusababisha baadhi ya maeneo kukosa huduma kwa kukosa mawasiliano kwa taasisi hizo.

Ameitaka TANROADS kuwasiliana na viongozi wa Wilaya na Halmashauri zote kubaini maeneo ya barabara yanayohitaji marekebisho na kuanza kutatua mara moja bila kusubiri wananchi waanze kulalamika.

Pia ameiagiza TANROADS kuanza kuyafanyia kazi maeneo ya miji inayokuwa kwa kasi kama Kibaigwa, Mbande, Bahi na Chalinze nyama kuyaboresha maeneo hayo kupunguza magari makubwa kupaki barabarani na kusababisha ajali za mara kwa mara.

Kwa upande wake kaimu meneja wa TANROADS Mkoa wa Dodoma Mhandisi Salome Kabunda, amesema kwa mwaka huu wa fedha wametengewa kiasi cha Bilioni 18,647,821, huku wakitarajia kujenga kilomita 1723.91 za barabara na madaraja makubwa na madogo 332.

Pia amebainisha kuwa wamepanga kuanza na maeneo korofi huku akibainisha changamoto kubwa ya barabara kuharibika mapema ni mifugo kupita katika barabara hizo, uvamizi katika hifadhi ya barabara na kutupa taka katika mitaro ya maji na kusababisha mitaro hiyo kuziba.

Nae mratibu wa TARURA Mkoa wa Dodoma Mhandisi Lusako Kilembe akibainisha kuwa wamepanga kujenga mtandao wa barabara wa kilomita 6996.25, na wanahitaji kiasi cha shilingi bilioni 135.56 kwa mwaka wa fedha 2021- 2022, na malengo yao ni kuboresha barabara zote kuhakikisha zinapitika.



No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...