Search This Blog

Sunday, July 5, 2020

Hekta 20,000 zatengwa kwa matumizi ya vitalu ranchi ya Ruvu

Serikali imetenga hekta elfu ishirini katika ranchi ya Ruvu kwa ajili ya kuwapatia wafugaji vitalu, hasa vijiji vinavyozunguka ranchi hiyo iliyopo wilayani Bagamoyo mkoani Pwani ikiwa ni sehemu ya utatuzi wa migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji.

Akizungumza mara baada ya kutembelea vijiji vya Fukayosi na Mkenge vilivyopo katika wilaya hiyo na kukagua eneo la mipaka ya vijiji hivyo na ranchi ya Ruvu inayosimamiwa na Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amesema maeneo hayo yaliyotengwa watapatiwa wafugaji wenye uhitaji kwa utaratibu maalum utakaowekwa na NARCO pamoja na serikali ya wilaya ya Bagamoyo.

Naibu Waziri Ulega ameutaka uongozi wa NARCO ambao umesema kuanzia Julai 15, 2020 wataanza kupokea maombi kwa wafugaji wenye uhitaji wa vitalu katika ranchi hiyo na kutaka wafugaji kutoingiza mifugo katika mashamba ya wakulima. Kwani serikali inatoa maeneo hayo ili kuondoa migogoro ya ardhi.

Kuhusu uhaba wa maeneo katika wilaya ya Bagamoyo, Naibu Waziri Ulega amewataka watu waliopatiwa maeneo makubwa katika wilaya hiyo kuyaendeleza, ni baada ya kubaini uwepo wa maeneo makubwa katika vijiji vya wilaya hiyo ambayo hayajaendelezwa na kuwafanya wakulima na wafugaji wa maeneo hayo kukosa sehemu ya kulima na kufuga.

Awali wananchi hao walimweleza Naibu Waziri Ulega kero kubwa waliyo nayo kuwa ni uhaba wa ardhi unaosababisha wafugaji kukosa malisho na kulisha mifugo yao katika mashamba ya wakulima na kusababisha migogoro isiyokwisha.

No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...