Search This Blog
Sunday, May 17, 2020
Maambukizi ya corona yafikia milioni 4.7 ulimwenguni
Wakati visa vya maambukizi vikiongezeka kwa zaidi ya milioni 4.7 kote ulimwenguni, nchini Yemen watu 500 wamekufa katika kipindi cha siku nane zilizopita kusini mwa mji mkuu wa taifa hilo Aden.
Wengi wa wagonjwa walikuwa na tatizo la upumuaji, hali inayoibua wasiwasi kwamba virusi vya corona vinasambaa kwa kiasi cha kutoweza kudhibitiwa, kuzidi vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoliacha taifa hilo katika hali mbaya.
Mchimbaji mmoja wa makaburi ameliambia shirika la habari la Associated Press kwamba hajawahi kuona idadi kubwa ya maiti katika mji ambao umeshuhudia mapigano makali wakati wa vita vilivyodumu kwa zaidi ya miaka mitano. Wengine wameripoti vifo zaidi ya kimoja, katika kipindi cha siku moja.
Watumishi wengi wa afya wanaokabiliwa na upungufu wa vifaa vya kujikinga wanaogopa kuambukizwa na vituo vingi vya afya mjini humo vimefungwa kwa kuwa watumishi wamekimbia na wengine wanawakataa wagonjwa. Maafisa na raia wanasema hata namba ya simu iliyotolewa na Umoja wa Mataifa ya kuomba msaada wa huduma ya upimaji majumbani kwa wanaohiswa kuambukizwa haipokelewi.
Hata hivyo, afisa mmoja katika hospitali ya Al-Kubi, Mehdi al-Dabi amesema kwa siku wanapokea hadi wagonjwa 230 na wanawahudumia kwa usawa. Alisema "tunapokea zaidi ya wagonjwa 230 kwa siku, baadhi yao wanahisiwa kuwa na maambukizi ya virusi vya corona na wao tunawalaza pia. Tunawahudumia sawa wagonjwa wote tunaowapokea."
Soma Zaidi:Kipato duni kigezo cha kupata virusi vya corona
Zaidi ya watu 314,000 wamekufa kote ulimwenguni kutokana na COVID-19 na zaidi ya milioni 4.7 wameambukizwa.
Nchini Ujerumani katika mji wa Cologne, watu 70 wanaoishi kwenye makazi ya wakimbizi wamegundulika kuambukizwa virusi vya corona. Watu 300 walifanyiwa vipimo na wale walioathirika walipelekwa kwenye makazi ya Mtakatifu Augustin, umbali wa saa moja kutoka Cologne.
Watu 60 ambao hawajaambukizwa walihamishiwa kwenye makaazi mengine.
Nchini Afrika Kusini kumeripotiwa visa vipya 1,160, idadi ya juu kabisa kuripotiwa kwa siku moja tangu mwezi Machi ambapo kulirekodiwa kisa cha kwanza. Wizara ya afya imesema, jimbo la Western Cape maarufu kwa utalii limerekodi takriban asilimia 60 ya idadi jumla ya visa nchini humo iliyofikia 15,515. Idadi ya vifo imeongezeka hadi 263
Huko Brazil, rais Jair Bolsonaro ameonyesha kupuuzilia mbali kanuni za kujitenga hapo jana, wakati taifa lake likikabiliwa na mripuko mbaya kabisa. Brazil imethibitisha idadi ya walioambukizwa ikipindukia ya Italia na Uhispania na taifa hilo sasa likiwa la nne kwa idadi kubwa ya maambukizi ulimwenguni. Wataalamu wanaonya huenda maambukizi yakawa ni zaidi ya 240,000.
Nchini Mexico, kumerekodiwa visa 49,219 hapo jana huku vifo vikifikia 5,177. Wataalamu wamesema taifa hilo limeshuhudia kuongezeka kidogo kwa maambukizi kuliko wastani wa kiulimwengu kutokana na maradhi yanayoongeza hatari ya kuambukizwa kama kisukari na uzito mkubwa.
Kiongozi wa kanisa Katoliki duniani Papa Francis ameziomba serikali kuajiri wauguzi wengi zaidi na kuwekeza kwenye mafunzo na mazingira ya kazi. Papa Francis amesifu kujitoa na ujasiri wa wauguzi akisema umuhimu wao umejidhihirisha kupitia janga hili la corona.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Punguza kilo tano kwa siku saba
NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...
-
Kiwanja kinauzwa kipo Dodoma Mahungu njia ya kwenda Singida kabala hujafika NALA. Kiwanja ni cha Makazi kinaukubwa wa Sqm 450 ( 15 X...
-
Akionekana kwa mara ya kwanza kwa umma tangu aondoke madarakani, aliyekuwa Rais wa Marekani Donald Trump ameweka wazi uwezekano wa kuwania...

No comments:
Post a Comment