
MAJINA ya mabeki wawili wa pembeni Kelvin Kijiri wa KMC na David Bryson wa Gwambina FC, yameingia kwenye rada za Simba na Yanga lakini wakati zikianza mikakati ya kuwanasa, walinzi hao wawili wamepata mchongo huko Ulaya. Kama mchongo huo utatiki basi unaweza kutibua mpango wa kujiunga na timu hizo kongwe.
Kijiri anayecheza beki wa kulia na Bryson beki wa kushoto, wamepata ofa ya kufanya majaribio na klabu ya KAA Gent inayoshiriki Ligi Kuu ya Ubelgiji.
Taarifa za uhakika ambazo gazeti hili limezipata kutoka kwa mawakala wa kimataifa wa soka nchini, zimefichua kuwa maskauti wa Gent ambao, tangu mwaka huu uanze wamekuwa wakiifuatilia kwa ukaribu Ligi Kuu Bara na wamekoshwa na uwezo wa Kijiri na Bryson.
“Wamekuwepo nchini tangu Januari na Kijiri wamemfuatilia katika mechi kadhaa za KMC na kuvutiwa naye zaidi baada ya kufahamu kuwa ana umri mdogo ambao, unaweza na faida kwao kumuuza siku za usoni na Bryson walimuona katika mechi ya Kombe la Azam Sports baina ya Yanga na Gwambina iliyochezwa Uhuru.
Kinachosubiriwa kwa sasa ni msimu umalizike ili watumiwe tiketi kwenda Ubelgiji kwa majaribio ambayo yatafanyika kwa muda wa mwezi mzima kwani, hakutokuwa na mechi za ligi ya Ubelgiji kwa kipindi hicho,” alisema wakala huyo.
Ikiwa mpango huo utatimia, ni wazi utaziweka katika wakati mgumu, Yanga na Simba ambazo zinatajwa kupigana vikumbo kuwawania mabeki hao wawili ili wajiunge nazo wakati wa usajili wa majira ya kiangazi.
Timu hizo zote mbili zinamuwania Kijiri zikimtazama kama mrithi wa kudumu wa mabeki wao wa kulia ambapo, kwa Simba anatazamwa kama mbadala wa Shomary Kapombe na upande wa Yanga kumpokea kijiti Juma Abdul.
Lakini, Yanga pia inatajwa kuwa na mpango wa kumsajili Bryson kwa ajili ya kucheza nafasi ya beki wa kushoto, namba tatu ambayo kwa sasa amekuwa akipangwa Japhary Mohamed ambaye kiasili ni kiungo.
Mbali na dili hilo la Gent, kihunzi kingine kwa vigogo hivyo viwili katika mchakato wa kuwasajili wachezaji hao ni mikataba ya muda mrefu ambayo wachezaji hao walisaini.
Akizungumza na gazeti hili, Bryson ambaye pia anahusishwa na Azam FC, alisema amesikia taarifa za kuhitajiwa na Gent na kuhusu mpango wa Yanga au Azam FC kumsajili amekuwa akisikia na kusoma kama tetesi.
Kwa upande wa Kijiri, uongozi wa KMC umeziita mezani timu zinazotamani kumsajili.
“Sisi kama KMC tuko tayari kumuuza ikiwa timu itakayomhitaji itafikia makubaliano na sisi na ikatoa dau ambalo linaridhisha vinginevyo ataendelea kucheza hapa kwa sababu anajisikia furaha,” alisema Mtendaji Mkuu wa KMC, Walter Harrison.
No comments:
Post a Comment