
BODI ya Ligi Kuu Bara, imesema Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka (TFF), ndiyo yenye mamlaka ya kuifuta ligi ama la lakini ikaibua kwamba, hakuna kanuni yoyote kwao inayotafsiri jambo hilo.
Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara, Almas Kasongo alisema, kama ambavyo walifanya hapo awali kamati ya utendaji ilikutana na kufanya kikao ambacho kilisimamisha ligi hivyo na kufanya maamuzi mengine ni lazima ikutane pia.
Alisema kitendo cha Shirikisho la Soka Uholanzi kufuta Ligi hiyo watakuwa wamejiridhisha kutokana na hali halisi iliyopo kwa sasa na kwamba, hata hapa mambo yakiendelea kuwa ndivyo sivyo watajua namna gani ya kufanya.
Kasongo alisema, kanuni hazisemi inapotokea janga kama la corona ama ishu yoyote juu ya ligi bali kanuni zinazungumzia mchezo tu, hivyo ni wakati muhimu kufanya maboresho ya kanuni kuliangalia jambo hilo.
“Kanuni zinasema mchezo na ndio maana kukiwa na mapungufu katika mchezo unaweza kusimamishwa au kufutwa ila kuhusu ligi mfano katika janga kama hili hakuna kanuni,” alisema Kasongo.
TFF imesisitiza kuwa hawawezi kufanya maamuzi yoyote mpaka wapate muongozo kutoka kwenye mamlaka za juu serikalini.
SIMBA WAPEWE
Viongozi wa matawi wa Simba na Yanga pamoja na timu mbalimbali za Ligi Kuu na Daraja la Kwanza wametofautiana kuhusu Simba kupewa ubingwa, ligi ifutwe ama ichezwe bila mashabiki pindi corona itapomalizika.
Katibu wa Simba Tawi la mkoani Mwanza, Philbert Kabago alisema ugonjwa huu ni mkubwa hivyo kinachotakiwa ligi hiyo iishie hapo na timu inayoongoza ipewe ubingwa huku zile ambazo zinatakiwa kushuka daraja zishuke ili mambo yaishe.
“Tukisema ligi ifutwe itakuwa hasara kwa timu kikubwa kama tayari imeshachezwa basi kwa sasa kiangaliwe nani anayeongoza apewe ubingwa na zile zinazotakiwa zishuke na kupanda uwekwe utaratibu mpya,” alisema Kabago.
Makamu Mwenyekiti wa Simba Mkoa wa Shinyanga, Idd Abas alisema; “Simba ana pointi nyingi, hivyo apewe Kombe kisha zile timu nne zinazofuata zichezeshwe Playoff kupata mshindi wa pili, wakati huo timu sita za chini zishindanishwe kupata nne za kushuka daraja.”
Naye Mwenyekiti wa Simba Mkoa wa Geita, Samwel Mizanza alisema; “Nashauri ligi iendelee lakini kama itaonekana kuna ugumu, Simba apewe ubingwa na zile timu mbili za Daraja la Kwanza zipande na yaani msimamo usibadilike sehemu zote.”
Mwenyekiti wa Yanga Tawi la Mwanza, Imani Madega alisema; “Kama ligi ikishindwa kumalizika na ubingwa akapewa Simba basi italeta malalamiko, niombe tuwe wavumilivu naamini huu ugonjwa utamalizika na mechi zitaendelea kupigwa ili mbabe wa kweli apatikane uwanjani.”
Naye mwanachama wa Yanga, Haruna Ramadhani alisema ni bora kusubiri kuliko kufuta ligi hiyo kwani italeta mkanganyiko kwa klabu zinazoshiriki mashindano hayo.
Katibu Mkuu wa Gwambina FC, Daniel Kirai alisema iwapo hali itakuwa tete kiasi cha kutoruhusu Ligi kuendelea, isimamishwe na hali ikitulia waendelee palepale.
“Yaani shule zikifunguliwa basi wanafunzi warudie madarasa? Haiwezekani ni bora kusubiri,” alisema.
Mwenyekiti wa Klabu ya Mbao FC, Solly Njashi alisema Ligi isifutwe isipokuwa wadau wawe wavumilivu.
Naye Kipa wa Azam FC, Benedict Haule alisema iwapo mambo yatazidi kuwa magumu; “Ligi ianze upya kama hali itakuwa mbaya sana au mamlaka ziangalie namna ya kuweka vituo ili kumaliza msimu na bingwa apatikane uwanjani kama zilivyo kanuni.”
IMEANDIKWA NA MASOUD MASASI, SADDAM SADICK NA CLEZENCIA TRYPHONE
No comments:
Post a Comment