
SIMBA hawaongei sana kuhusiana na ishu za usajili mpya, lakini uchunguzi wa Mwanaspoti umebaini kuna mambo wanafanya chini kwa chini na yakiibuka kishindo chake ni kizito.
Tayari wekundu hao wamerudisha majeshi kwa straika Mburkina Fasso, Songne Yacouba (29) ambaye ameachana kwa mbinde na Asante Kotoko ya Ghana baada ya mkataba wake kumalizika hivi karibuni huku akiwa na sifa moja tu ya ukali wa asisti zake. Ukiacha za kwenye Ligi ya Ghana, katika Kombe la Shirikisho msimu uliopita alikuwa na asisti tano na bao mbili mpaka timu yake inatolewa.
Asante Kotoko walimtaka mchezaji huyo kusaini mkataba mpya ili wamuuze kwa bei ghali kwa Simba au Orlando Pirates ya Afrika Kusini, lakini akazira jambo ambalo lilimpa wakati mgumu kwenye wiki za mwisho kwani aliambulia kusugua benchi.
Awali msimu uliopita Simba walipewa jina la mchezaji huyo na kocha wa wakati huo, Patrick Aussems akajiridhisha kwamba ni mashine kwelikweli , ila ishu ikaja kwenye dau lake binafsi na klabu yake kwa vile bado alikuwa na mkataba mrefu.
Habari zinasema kwamba Simba kwa sasa chini ya Ofisa Mtendaji Mkuu, Senzo Mazingisa wameshawasiliana na wakala wa mchezaji huyo na dili hilo liko kwenye hatua nzuri, ilhali uwezekano wa kutua Msimbazi msimu ujao ni mkubwa na anakuja kama mchezaji huru ingawa huenda Simba ikalazimika kumpa Sh340 milioni anazotaka japo inadaiwa makubaliano yapo.
Simba wanaamini kwamba umahiri na utayari wa straika huyo kimchezo utawanufaisha kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika watakayoshiriki baadaye mwaka huu.
Habari za uhakika kutoka ndani ya Simba zinasema kuwa tayari wameshajiridhisha kwamba mchezaji huyo atawafaa na Kocha Sven amemkubali zinazoendelea sasa ni taratibu za kiofisi tu na huenda akawa mchezaji wa kwanza kumwaga wino Simba baada ya Coastal Union kupandisha thamani ya beki wao, Bakary Mwamnyeto.
Kocha wa Simba anataka aletewe straika wa maana atakayesaidiana na Mnyarwanda Meddie Kagere kwenye kutupia ambapo ni Mburkinafasso huyo alikuwa akihusishwa pia na Medeama FC ya Ghana iliyoshindwa dau lake.
Sven mwenyewe Mwanaspoti linafahamu kwamba alishaanza kutafuta mshambuliaji wa kati na wakala mmoja maarufu anayetumiwa na Simba ameliambia Mwanaspoti kuwa Yacouba amemaliza mkataba na Kotoko na amegoma kusaini kwa vile ishu yake na Simba imeiva na anataka kubadili upepo kujiunga na klabu yenye mtazamo wa kimataifa.
“Simba wanajadiliana, kama wakikubaliana bei yake nafikiri watarudisha jibu kwa kumalizia tu, sioni kama bei aliyowapa wataishindwa kwa alivyo tajiri na uhitaji. Ni mshambuliaji mwenye hadhi ya kuipa Simba mafanikio hata katika Ligi ya Mabingwa Afrika endapo watakuwa mabingwa tena,” alisema wakala huyo.
Mapema mwanzo wa msimu huu Yacouba aliwahi kuja nchini na Kotoko kisha kukubalika katika mchezo wa Wiki ya Simba, na kwa akili na nguvu aliwasumbua mabeki wa timu hiyo.
Uwezo wake huo ulimkosha aliyekuwa kocha wa Simba Patrick Aussems.”
Yacouba alijiunga na Kotoko mwaka 2018 na baada ya mkataba wake kumalizika ameamua kutulia zake huku mitandao ya Ghana ikidai kwamba akili yake ni kwenda barani Asia baadaye mwaka huu ndio maana anatafuta sehemu asaini mkataba wa muda mfupi.
No comments:
Post a Comment