
MASTAA wawili waliowahi kutamba na kuacha alama ndani ya Yanga, Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ na Zamoyoni Mogella ‘Golden Boy’ wamesikia tambo za Kocha Luc Eymael kuhusiana na usajili mpya wa msimu ujao, lakini wakongwe hao wamempa vigezo na mapendekezo yao.
Wamesisitiza kwamba vigezo ni vigumu, lakini kama Yanga inahitaji mabadiliko ya kiuchezaji na kupiga hatua lazima itafute mashine ambazo zinaweza kuvuka vihunzi hivyo na barani Afrika wapo wengi kama umakini utaongezwa.
Mmachinga alisema wachezaji ambao wanataka kusajiliwa na ‘Yanga ya GSM’ wawe na tija na watakaokwenda kucheza na kutoa mchango wao katika kikosi cha kwanza badala ya kuishia jukwaani tu na kusingizia majeraha na hali ya hewa.
“Yanga wanatakiwa kusajili wachezaji wawe wazawa au wageni, lakini waingie katika kikosi cha kwanza na kwenda kutoa mchango wao katika timu ili kufikia malengo yao ambayo watakuwa wamejiwekea,” alisema Mmachinga.
Mogela ‘Golden Boy’ alisema, “kwanza hao wachezaji wa kigeni katika mikataba yao kunatakiwa kuwepo na vipengele ambavyo vinaonyesha mambo ambayo wanatakiwa kuyafanya na kama ikiwa tofauti na hivyo mkataba wake unaweza kuvunjwa hasa kwenye nafasi ya ushambuliaji ambako ndiko paliko na mtihani miaka mingi.
“Kama anasajili straika wa kigeni katika mkataba wake ndani ya msimu uonyeshe wazi kwa maandishi kwamba anatakiwa kufunga mabao fulani ambayo asipofikia hayo ionyeshe kabisa hajatimiza lengo na mkataba wake unaweza kuvunjwa.
“Nadhani jambo kama hilo litasaidia kuwa na usajili mzuri si kwa Yanga tu, bali timu zote na hao wachezaji ambao watasajili watakuwa wanajituma kufikia malengo yao na kiwango cha soka letu kitaimarika, hakutakuwa na mzaha.”
Mchezaji wa zamani wa Mtibwa Sugar na Yanga, Vicent Barnabas alisema Yanga wanatakiwa kufanya usajili kulingana na upungufu wao na sio fasheni ili kukwepa jambo ambalo wamekutana nalo msimu huu kusajili wachezaji wengi katika madirisha mawili ambao wameshindwa kufanya vizuri.
“Yanga wanatakiwa kuwa na utulivu na kufuatilia vya kutosha upungufu wao na kuona wachezaji gani ambao wana sifa ya kwenda kuziba upungufu huo na kufanya vizuri msimu ujao, lakini kama ikiwa tofauti na hivyo hawataweza kuziba upungufu wao wa msimu huu,” alisema mchezaji huyo ambaye wakati anacheza Yanga alikuwa na nywele ndefu ambazo mashabiki wa Simba walikuwa wakimkejeli kwamba ni wigi na zinamfanya ainamishe uso chini anavyojiandaa kupiga majalo.
Kocha wa Yanga, Luc Eymael amesisitiza kwamba kwenye usajili wake mpya anataka wachezaji wa kazi na ambao wataleta mabadiliko makubwa kwenye kikosi cha kwanza na kubadili staili yake ya uchezeshaji.
Amesisitiza kwamba kazi hiyo anaifanya kimyakimya, lakini anataka wachezaji kasi zao hususan kwenye winga, viwango bora na umri mdogo kwenye kila eneo huku akimtaja mzawa mmoja tu aliyepo katika mipango yake ambaye ni Zabona Khamis wa Alliance na tayari ameshawapa viongozi jina lake.
No comments:
Post a Comment