
Dar es Salaam. Dakika 90 za mchezo wa ugenini dhidi ya Polisi Tanzania leo, zinaweza kuipandisha Namungo FC hadi nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Ushindi katika mchezo huo utakaochezwa kwenye Uwanja wa Ushirika mjini Moshi, utaifanya Namungo FC kufikisha pointi 50 na kusogea hadi nafasi ya pili mbele ya Azam na Yanga.
Hata hivyo, hilo litatimia ikiwa tu Azam FC yenye pointi 48 itatoka sare au kupoteza mchezo wake dhidi ya Alliance FC utakaochezwa kwenye Uwanja wa Taifa leo saa 1.00 usiku.
Lakini kama Azam FC itaibuka na ushindi dhidi ya Alliance, wataendelea kubaki katika nafasi ya pili waliyopo sasa.
Ikiwa timu hizo mbili zote zitapata ushindi, Namungo atakaa katika nafasi ya tatu kwa muda kungojea matokeo ya mechi ya watani wa Jadi itakayochezwa kesho na ikiwa Simba itaibuka na ushindi dhidi ya Yanga, Namungo itasogea hadi nafasi ya tatu.
Na bado Namungo itabakia na faida ya kuwa na mechi moja ya kiporo dhidi ya Yanga ambayo bado haijapangiwa tarehe.
Hata hivyo, haitokuwa kazi rahisi kwa Namungo FC kwani wanakutana na Polisi Tanzania ambayo imetoka kujeruhiwa kwa kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Mwadui FC na imekuwa mwiba mkali kufungika nyumbani.
Kocha wa Namungo, Hitimana Thiery alisema wanatambua ugumu wa mechi hiyo na wamejiandaa kukabiliana nao.
“Polisi ni timu nzuri na imekuwa ikicheza soka la ushindani hivyo tunatarajia haitokuwa mechi rahisi ingawa tumejipanga kushinda katika mchezo huo,” alisema Thiery.
Mechi nyingine za leo, ni Singida United v Prisons, Ruvu Shooting v JKT Tanzania, Coastal Union v Ndanda FC, Lipuli v Biashara, Mtibwa v Kagera Sugar, KMC v Mbao FC na Mwadui itakuwa kule Mwadui Complex kucheza dhidi ya Mbeya City.
No comments:
Post a Comment