
NI zaidi ya mbio! ndivyo wakazi wa Mji wa Moshi na maeneo jirani wanavyozitizama mbio za Kilimanjaro Marathoni maarufu kama Kili marathoni.
Jumapili iliyopita mbio hizo zilifanyika kwa mara nyingine ikiwa ni msimu wa 18 tangu zilipofanyika kwa mara ya kwanza mwaka 2003 zikidhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia ya Kilimanjaro Premium Lager.
Kila mwaka mbio hizo hufanyika kwenye viwanja vya Ushirika mjini Moshi huku mchuano mkali ukiwa kwa nyota wa Tanzania na Kenya.
Mwaka huu, wanariadha 800 walichuana katika mbio za marathoni (kilomita 42) ambazo hudhaminiwa na bia ya Kilimanjaro, 5500 walichuana mbio za Tigo nusu marathoni (kilomita 21) ambazo udhaminiwa na kampuni ya simu ya Tigo na 4500 walishiriki zile za Grand Malt fun run za kilomita tano.
Mambo yalivyokuwa uwanjani
Mbio hizo ambazo huandaliwa na Kampuni ya Wild Frontiersn hufanyika Machi kila mwaka na mwaka huu zilifanyika Machi Mosi zikianzia Uwanja wa Ushirika kupitia barabara ya Kili, KCMC, Mwika Masoka, Soweto, TPC na kurudi uwanjani.
Tanzania iliingiza wanariadha saba kwenye 10 bora ya mabingwa kwa wanaume waliokimbia nusu marathoni na kutwaa medali ya dhahabu kwa wanaume na wanawake zilizochukuliwa na Joseph Panga aliyekimbia kwa saa 01:03:59 na Magdalena Shauri aliyekimbia kwa saa 01:09:54.
Josephat Joshua alitwaa fedha kwa wanaume katika nusu marathoni, wakati Vicent Towett wa Kenya akitwaa shaba, Susy Chebet na Valentine Jepkorir wote kutoka Kenya walitwaa medali ya fedha na shaba kwa wanawake.
Kwenye marathoni (kilomita 42), Wakenya, Kiplagat Kiplimo, Abraham Too na Bernard Kipchirchir walitwaa medali ya kwanza hadi ya tatu kwa wanaume na wanawake Lydia Wafula, Rosina Kiboino na Joan Rotich pia wa Kenya walitwaa medali.
Nje ya mbio mambo yalikuwa hivi
Wenyeji wa mji wa Moshi wanasema, pilika pilika zinazoashiria kuanza kwa mbio hizo huanza wiki moja kabla kwa maeneo mengi ya mji huo kupambwa na mabango yanayoashiria uwepo wa mbio hizo kubwa za fedha nchini na wageni kuanza kuwasili.
Siku mbili kabla ya kuanza kwa mbio hizo, mji huo huzizima kwa wageni.
“Ndicho kipindi cha kufanya biashara, unaweza kupata faida mara 50 zaidi ya siku nyingine za kawaida,” anasema dereva wa bodaboda aliyejitambulisha kwa jina moja la Shayo.
Kumbi mbalimbali za burudani, nyumba za kulala wageni na maeneo ya migahawa hufurika wageni waliokwenda kwa lengo la kushiriki mbio hizo na baadhi ya wenyeji ambao hawabaki nyuma kipindi hicho.
“Mwaka 2019, zaidi ya watu 20,000 walishiriki mbio hizi, mwaka huu rekodi imevunjwa tumekuwa na watu zaidi ya 30,000,” alisema Mkurugenzi wa mbio, John Bayo.
Wenyeji wanasema siku moja kabla ya mbio hizo, nyumba za kulala wageni ndani na nje ya mji wa Moshi zinajaa na wakati mwingine baadhi ya watu hukodisha nyumba zao kwa wageni.
“Kama usipoweka oda mapema, ni ngumu kupata chumba, wageni wengi huwa wanawatumia wenyeji walioko huku na kulipia kabisa kabla hawajafika, ukichelewa, siku moja kabla ya mbio kupata chumba ni nadra, labda ulale kwenye vile vya kuanzia Sh100,000 na kuendelea lakini chini ya hapo ni bahati kupata,” anasema mkazi mwingine wa mji huo.
Vyakula, usafiri bei juu
Ukiachilia mbali nyumba za wageni za kawaida ambazo bei yake ni kati ya Sh7000 hadi 30,000, wakati wa mashindano hayo, bei hizo hupanda na kuwa mara mbili hadi mara tatu.
Kwenye vyakula nako mambo huwa hivyo hivyo, huku wenyeji wanaojua kutumia fursa wakisema biashara inakuwa nzuri hivyo kulazimika kukesha wakipiga pesa.
“Hii ndiyo fursa ya kupata pesa, binafsi kipindi cha Kili Marathoni huwa silali na biashara haidodi,” anasema mfanyabiashara wa chakula, Haines John.
Madereva bajaji na bodaboda licha ya bei ya kawaida kuwa Sh500 mpaka 1000 kwa safari za mjini, kipindi cha mashindano hayo bei hiyo huwa mara mbili, huku wakipanga na bei za usiku na Alfajiri.
Rekodi ya 2020, haijawahi kutokea
Mkurugenzi Mkuu wa Executive Solutions ambao wanaratibu mbio hizo kwa upande wa vyombo vya habari, Aggrey Marealle anasema tangu zilipoanza mwaka 2003, zimekuwa zinaongezeka umaarufu kila mwaka.
“Ukiachana na ushiriki wa wanariadha wa Tanzania waliofanya vizuri mwaka huu, pia zimekuwa kivutio kwa wageni na wenyeji pia.
“Kila mwaka washiriki huongezeka, watu wanaovutiwa kuja kushiriki ni wengi na tunatarajia rekodi hiyo iendelee kuvunjwa miaka ijayo,” alisema Marealle.
Nyota wa Tanzania wafunguka
Licha ya Wanariadha kutoka Kenya kung’ara kwenye mbio za kilomita 42 kwa muda mrefu, nyota wa Tanzania msimu huu wametakata kwenye mbio za nusu marathoni na Tanzania ilivuna medali zote mbili za dhahabu kwa wanaume na wanawake na fedha kwa wanaume.
“Ni mbio zenye ushindani, kama huna mazoezi huwezi kukimbia na kushinda, binafsi nilipambana na sikuruhusu kupitwa na Mkenya tangu mbio zinaanza hadi namaliza na kutwaa ubingwa,” alisema Joseph Panga bingwa wa nusu marathoni kwa wanaume.
Nyota wa Tanzania upande wa wanawake, Magdalena Shauri alisema mbinu na maandalizi ndivyo vilimbeba mbele ya Wakenya watano waliokuwa wakienda naye sambamba.
No comments:
Post a Comment