Search This Blog

Tuesday, March 3, 2020

DC ashangaa wafu kumdhamini karani


MKUU wa Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera, Deodatus Kinawilo, ameshangazwa na kitendo cha karani wa Chama cha Msingi cha Ushirika Kaibanja, Sweetbert Mutembei, kudhaminiwa na watu waliofariki dunia.

Kiongozi huyo amepigwa na butwaa baada ya kufuatilia malalamiko ya wakulima wa kahawa kutolipwa fedha zao na chama hicho kwa kipindi cha zaidi ya miezi sita, huku sehemu ya kahawa inayodaiwa kukusanywa na wakulima hao ikiwa haiko ghalani.

"Sijawahi kuona maishani mwangu, mtu anadhaminiwa na watu waliokufa kazini, karani huyu anatuhumiwa kuhujumu kahawa ya wakulima, haonekani lakini nilipofuatilia waliomdhamini kwa kazi hii, wote ni marehemu. Ofisa ushirika huu ni uzembe wa hali ya juu," alisema.

Kinawilo alisema kitendo cha karani huyo kudhaminiwa na watu waliofariki dunia kimetokana na uzembe wa Ofisa Ushirika, Mutawajibu Rwiza, na kumwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, kumpangia kazi nyingine.

"Alitakiwa kuhakikisha kwamba karani huyo anadhaminiwa na watu walio hai, wote hawa wamefariki, yaani wafu wanamdhamini vipi karani? Kumdhamini kwao kunaonyesha hakukuwa na umakini kwa ofisa ushirika," alilalamika.

Alisema uchunguzi alioufanya kwa kushirikiana na uongozi wa Chama Kikuu cha Ushirika mkoani Kagera (KCU 1990 LTD), umebaini kuwapo kwa upotevu wa tani 25 za kahawa yenye thamani ya Sh. milioni 28.

Mkuu wa Wilaya huyo aliitisha mkutano wa dharura na wakulima wa zao la kahawa katika eneo hilo, uongozi wa Chama cha Ushirika cha Msingi Kaibanja na uongozi wa KCU.

Wakati mkutano huo ukiendelea, kiongozi huyo wa wilaya aliwakabidhi viongozi wanne wa chama hicho cha msingi kwa Mkuu wa Kituo cha Polisi Wilaya ya Bukoba kwa uchunguzi, lakini karani aliyekuwa analalamikiwa, hakuwapo.

"Karani huyu ambaye ametoweka na hapa hayupo, naomba asakwe popote pale alipo, aletwe kujibu tuhuma zinazomkabili na upotevu wa kahawa ya wakulima, lakini hawa wanne, OCD ondoka nao uwahoji, dhuruma kwa wakulima kwa awamu hii haikubaliki," alisema.

Alisema serikali inajitahidi kukusanya mapato ya ndani ili kupunguza kero za wananchi wakiwamo wakulima wa kahawa, lakini wanatokea watu wachache wasio waaminifu na kula fedha za wakulima.

Mkaguzi wa Ndani wa KCU aliyefanya ukaguzi na kubaini upotevu huo wa kahawa, Robert Kateka, alisema ukaguzi uliofanyika ulibaini uwapo wa wanachama wanaokidai chama hicho zaidi ya Sh. milioni 28.

"Ukaguzi umebaini kuwapo kwa upungufu wa kahawa katika ghala zaidi ya kilogramu 25,000 ambayo thamani yake ni zaidi ya Sh. milioni 28.

No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...