
TANGU zama za kale binaadamu amevumbua michezo ya aina mbalimbali ili kuupa mwili mazoezi kwa ajili ya kuimarisha afya yake au kupata burudani.
Kila siku zikipita aina mbali mbali ya michezo hufanyika kwenye viwanja, ndani ya majengo, maji ya bahari, kwenye matope, kwenye misitu, milima, barafu na kwengineko. Lakini baadhi ya michezo iliyovumbuliwa karne iliyopita na hasa katika miaka ya karibuni unaweza kusema ni ya vioja vya aina yake na kwa kweli ipo ambayo sitaweza kuigusia kwa vile haikubaliki kuelezewa hadharani kwa utamaduni wetu.
Miongoni mwa michezo iliyonishangaza ni ya mtu aliyeutumia ulemavu alionao kuvumbua mchezo uliomfanya kuwa na maisha bora na kuwa kivutio kikubwa kila alipokwenda.Huyu ni raia wa Angola, Francisco Domingo Joaquim, ambaye sasa ana umri wa miaka 30 mwenye mdomo mpana sana na kutambulika kuwa ni mwenye upana mkubwa wa mdomo kuliko mtu yoyote duniani.
Hali hii ya Franscisco imetokana na matatizo aliyonayo ya mishipa dhaifu ya eneo linalozunguka mdomo, mashavu na kidevu chake. Upana wa mdomo wake ambao umekaa kama mpira ni sentimita 16.99) (inchi saba). Huyu jamaa ameugeuza ulemavu wake huu wa mdomo kuwa ni kitega uchumi ambacho kimemfanya kuwa na maisha mazuri, ya raha na furaha.
Kwa mfano, anapotembelea Ulaya mtu anayetaka apige picha naye humtoza ada ya kati ya dola za Kimarekani 30 hadi (Shilingi 70,000) hadi dola 100 (Shilingi 230,000) na anayetaka hiyo picha iwe anampiga busu basi lazima alipe zaidi. Hodi, sio madogo haya!
Amekuwa akishinda mashindano yote aliyoshiriki ya kutafuta watu wenye midomo mipana na kufanya mambo yasiyo ya kawaida kwa kutumia mdomo.
Ushindi wake maaarufu wa kwanza ulikuwa mwaka 2010, akiwa na miaka 20, alipoonyesha utaalamu wa kuchezea mdomo wake katika mashindano ya kimataifa ya Domo Kubwa (Big Mouth) yaliyofanyika Rome, Italia.
Francisco ambaye anajulikana zaidi kama Taya ya Angola anaweza kutia mdomoni na kukichezesha kikopo cha soda bila ya matatizo. Katika mashindano ya Rome wakati wenzake walikuwa wanachukua vipande viwili au vitatu vya keki kutia mdomoni yeye alikuwa akibeba 10 pamoja na kutia mdomoni glasi na vikombe bila ya matatizo.
Vituo vingi vya runinga vya Italia na nchi nyingine za Ulaya huwa vinamualika kwa donge nono kufanya maonyesho na kampuni nyingi humwita kufanya hivyo na kutoza fedha wanaopanda kwenye jukwaa kucheza naye au kupigwa busu. Moja ya rekodi zake maarufu ni kutia mdomoni na kutoa mara 14 kopo la soda kwa muda wa dakika moja.
Mara nyingi amefanya maonyesho kupitia vituo vya runinga vya Luanda, kumbi mbali mbali na wakati mwingine barabarani na kufanya maonyesho na kurudi nyumbani na kitita cha fedha.
Amekuwa akisema: “Serikali ya Angola inategemea mafuta kujiendesha. Mimi natega mdomo wangu mpana’.
Mchezo mwengine ambao hufanyika katika baadhi ya nchi za Afrika, Asia ni wa kuweka masega ya nyuki na washiriki kuyavamia.
Mshindi ni yule anayepatikana mwilini na ‘sindano’ nyingi za kutafunwa na nyuki. Hata hivyo, kwa sasa hakuna aliyeifikia rekodi iliyowekwa Januari 28, 1962 na Johannes Relleke wa Rhodesia ya Kaskazini (sasa Zimbabwe) ambaye alitafunwa na nyuki 2,443 na kubaki hai baada ya sindano hizo kutolewa mwilini.
Mashindano mengine yanayopendwa sana siku hizi ni ya wazee wa zaidi ya miaka 60 na zaidi kutambaa kwa masafa ya kati ya mita 100 hadi 400. Waandaaji wa mashindano haya yanayovutia watu wengi wanasema washiriki hujikumbusha walivyokuwa wakitambaa walipokuwa wadogo.
Mbio za kutambaa kama mtoto mdogo kabla hajainua miguu kwenda au kama konokono. Siku hizi pia mchezo wa mieleka wa kutumia vidole vya mguu. Katika mchezo huu washiriki hupanda juu ya jukwaa na wakiwa wamelala chini kisha kila mmoja huvisokota vidole vya mpinzani wake ili apate maumivu makali au hata avivunje ili aibuke mshindi. Huu ni mchezo mingine wa kiwendawazimu.
Siku hizi vipo vyama vya michezo katika baadhi ya nchi vinavovyojikita katika mapenzi. Miongoni mwa malengo yao makubwa kwa kushirikiana na vyama vya riadha huandaa mashindano ya mbio ambayo washiriki wake huwa wanaume waliowabeba wake zao mgongoni au wanawake waliowabeba waume zao mgongoni.
Miongoni mwa masharti kwa washiriki ni kutoa vielelezo, hasa cheti cha ndoa, kuwa huyo unayekwenda naye katika mashindano ya hayo ni mwanandoa wako kweli. Mchezo huu wa kumbeba mwandani wako mgongoni na kukimbia naye unapendwa sana Finland. Kama mzee mwenye mke mnene na mzito sana anataka kushiriki ili kuonyesha hadharani mahaba hiyo ni shauri yake.
Mashindano mengine ya kiwendawazimu ni ya kuvuana viatu. Katika mchezo huu washiriki hupewa aina moja ya viatu, lakini kwa kulingana na urefu wa miguu yake.
Mchezo huwa na washiriki wawili wawili. Kila mmoja baada ya kuvifunga vizuri nyuzi kwa njia atakayo, lakini isiyo na utata wa kuweza kufunguka kwa kutumia vidole hupulizwa filimbi.
Hapo tena huanza pambano la kila mmoja ajitahidi kumvua viatu mwenzake. Anayetangulia kumvua kiatu kimoja anayepambana naye ndio mshindi. Katika hii orodha ya michezo ya aina yake ni ya washiriki kuingia kwa wakati mmoja katika bwawa la samaki wadogo.
Mshiriki anayefanikiwa kumkamata samaki haraka ndiye mshindi.
No comments:
Post a Comment