Search This Blog

Monday, December 16, 2019

Makocha hawa Ligi Kuu hawataisahau 2019

By Mwandishi wetu

WAKATI mwaka 2019 ukikaribia kumalizikia mambo yamekuwa si mambo kwa upande wa makocha wanaozinoa baadhi ya timu za Ligi Kuu Bara.

Mwaka huu umeongoza kwa makocha kutimuliwa katika klabu walizokuwa wakizifundisha, hivyo kuufanya kuwa mwaka mbaya zaidi kwa makocha wengi tofauti na miaka ya nyuma.

1.Hans Pluijm- Azam.

Kocha huyu wa zamani wa Yanga alijiunga na Azam FC Juni, mwaka jana, kama kocha mkuu pamoja na Juma Mwambusi aliyekuwa msaidizi. Kocha huyo aliiongoza Azam hadi Februari, mwaka huu alipotimuliwa kwa madai ya matokeo yasiyoridhisha.

Kipigo cha mabao 3-1 ilichokipata Azam kutoka kwa Simba, Februari 22, mwaka huu, ndicho kilichohitimisha kibarua cha kocha huyo pamoja na msaidizi wake Mwambusi, kwani kabla ya mchezo huo alishindwa kupata matokeo mazuri katika mechi nne mfululizo baada ya kuambulia pointi tatu kutokana na kupata sare katika michezo mitatu huku akipoteza mmoja.

Pluijm aliiacha Azam ikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi kwa pointi 50 nyuma ya Yanga iliyokuwa na pointi 61.

Advertisement

2.Mwinyi Zahera- Yanga

Kocha huyu raia wa DR Congo alitimuliwa pamoja na benchi lake lote la ufundi, Novemba 5 na kuwaacha mashabiki wa klabu hiyo wasiamini wanachokisikia.

Zahera ambaye alisifika kwa kusema ukweli pale kitu kilipomkwaza aliondolewa ndani ya klabu hiyo bila viongozi kuweka wazi sababu jambo ambalo liliwafanya mashabiki na wadau wa soka kujiuliza maswali bila majibu.

Kocha huyo ambaye inadaiwa alikuwa akitoa fedha zake mfukoni kuisaidia timu hiyo alivunjiwa mkataba wakati akiwa mazoezini akiendelea na majukumu yake ya kuiandaa timu yake iliyokuwa ikijiandaa na mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Ndanda FC.

3.Patrick Aussems- Simba

Kuondoka kwa kocha huyu ndiko kulikoacha maswali mengi yasiyo na majibu kutoka kwa mashabiki na wadau wa soka kwani wengi waliona kama ameonewa.

Licha ya Simba kuongoza Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 25 tofauti ya pointi saba na wapinzani wao wakubwa, Yanga wenye pointi 17 lakini uongozi wa Simba ukaamua kuvunja mkataba na kocha huyo Mbelgiji maarufu kama Uchebe Novemba 30.

Kocha huyo ambaye aliiongoza Simba kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa msimu uliopita inasemekana pia kutolewa katika hatua za awali za mashindano hayo msimu huu kumechangia kung’olewa katika nafasi yake kwani timu haikuonyesha kucheza kwa kiwango kinachoridhisha.

Taarifa kutoka katika uongozi wa Simba zilisema wamemuondoa baada ya kufanya vibaya katika mechi za msimu huu za Ligi ya Mabingwa Afrika huku akishindwa pia kusimamia nidhamu ya wachezaji.

4.Athuman Bilal ‘Billo’- Alliance

Kati ya makocha walioweka rekodi ya kutimuliwa mapema zaidi msimu huu, basi ni huyu Athuman Bila ‘Bilo’ kwani aliiongoza Alliance FC katika mechi moja tu baada ya hapo akapewa mkono wa kwaheri.

Billo alitua Alliance FC Julai, mwaka huu na kusaini mkataba wa miaka miwili wa kuinoa timu hiyo akichukua nafasi ya Malale Hamisini, lakini akadumu kwa miezi miwili na kuondolewa.

Kocha huyo alitimuliwa baada ya kupata sare ya bao 1-1 dhidi ya Mbao FC katika mchezo wa kwanza wa ufunguzi wa Ligi Kuu Bara msimu huu jambo ambalo liliwashangaza wengi na pia kumuacha na mshangao hata yeye mwenyewe.

Baada ya kutimuliwa, Bilo alikaririwa akisema sababu kubwa iliyofanya uongozi kumuondoa ni kutotaka kuingiliwa katika majukumu yake hasa katika upangaji wa kikosi huku chanzo kikubwa ikiwa ni kufanya mabadiliko ya kumtoa Jerry Tegete katika mchezo dhidi ya Mbao FC na ndipo walipotofautiana na meneja wa timu hiyo.

5.Malale Hamsini -Alliance/Ndanda

Kocha huyu ambaye amekuwa mara nyingi akiifundisha Ndanda ya Mtwara, msimu huu amezunguka katika timu mbalimbali ikiwemo Ndanda ambayo aliinoa hadi Novemba, mwaka jana alipojiunga na Alliance FC.

Alidumu na Alliance FC kwa miezi sita na kuiwezesha timu hiyo kumaliza ligi msimu uliopita ikiwa nafasi ya 11. Hata hivyo, Julai mwaka huu alifungashiwa virago.

Malale alirejea tena Ndanda mwanzoni mwa msimu huu lakini akadumu miezi mitatu kabla ya kutimuliwa kwa madai ya matokeo mabaya ya timu na sasa ametua Polisi Tanzania kuchukua nafasi ya Seleman Matola aliyetimkia Simba.

6.Jackson Mayanja- KMC

Alijiunga na KMC Juni mwaka huu akichukua nafasi ya Mrundi Etienne Ndayiragije ambaye alitimkia Azam FC.

Hata hivyo, akadumu ndani ya kikosi hicho kwa miezi mitatu ambapo mwezi uliopita (Novemba) akatimuliwa kwa madai ya matokeo mabaya ya timu hiyo inayomilikiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni.

Mayanja, raia wa Uganda ametimuliwa KMC akiwa ameiongoza timu hiyo katika mechi sita za Ligi Kuu akishinda moja, sare mbili na kupoteza michezo miwili huku pia akipoteza mchezo mmoja wa kimataifa wa Kombe la Shirikisho barani Afrika dhidi ya AS Kigali ya Rwanda baada ya kutoka suluhu ugenini na kupoteza nyumbani kwa mabao 2-1.

Katika mchezo wa saba wa ligi ambao KMC ilishinda kwa mabao 2-1 dhidi ya Biashara United, Mayanja hakuwepo benchi kama ilivyokuwa katika mchezo waliochapwa mabao 2-1 na Kagera Sugar na ndio siku uongozi wa timu hiyo ulipotangaza rasmi kuachana na kocha huyo Mganda.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Bodi ya KMC, ambaye pia ni Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Benjamin Sitta waliamua kuachana na Mayanja kutokana na maendeleo yasiyoridhisha ya timu tangu kuanza kwa msimu.

Hata hivyo, sababu kubwa iliyochangia KMC kuanza ligi vibaya na kumuingiza matatizoni Mayanja ni kutokana na wimbi kubwa la wachezaji majeruhi lililokuwa likiikabili timu hiyo.

7.Amri Said- Biashara United

Alianza kuinoa Biashara United Januari, mwaka huu akichukua mikoba ya Hitimana Thiery aliyetimkia Namungo FC ya Ruangwa mkoani Lindi.

Amri alipata kibarua cha kuinoa Biashara United akitokea Mbao ya Mwanza ambayo aliifundisha mwaka jana, lakini akaikacha timu hiyo baada ya kuletewa kocha Ally Bushiri, hivyo akaona isiwe tabu ni bora aondoke kuliko kufanya kazi chini ya kocha huyo.

Hata hivyo, Septemba 26, mwaka huu akatimuliwa Biashara United baada ya kuiongoza timu hiyo katika mechi nne za msimu huu wa ligi huku akipoteza mechi tatu na sare moja.

Kwa sasa Amri amepata kibarua kingine baada hivi karibuni kutangazwa kuwa kocha mkuu wa Mbeya City akichukua nafasi ya Juma Mwambusi.

8.Fred Felix Minziro -Singida United

Amekuwa na bahati mbaya sana kwa timu ambazo amekuwa akzipandisha kucheza Ligi Kuu baada ya kufika huko tu, basi wanaachana naye.

Amewahi kufanyiwa hivyo na Singida United na hata KMC kwani aliziwezesha kupanda lakini malipo yake waachana naye na kutafuta makocha wengine.

Baada ya kuondoka kwa kocha Dragon Popadic, Singida United ilimkabidhi mikoba Minziro ambaye aliongoza hadi Oktoba, mwaka huu apoondolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Mrundi Ramadhan Nsanzurwimo.

Baada tu ya kutemwa Singida United, Oktoba 19, Minziro akatangazwa kuwa kocha mkuu wa Pamba FC ya Mwanza inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza

9.Juma Mwambusi- Mbeya City

Ni mmoja ya makocha bora hapa nchini ambapo alianza kufahamika zaidi mwaka 2013 wakati akiinoa Mbeya City iliyotikisa Ligi Kuu Bara.

Kufanya vizuri kwa Mbeya City kulimpa ulaji Mwambusi ambapo 2015 alijiunga na Yanga kama kocha msaidizi chini ya kocha mku Hans Pluijm na baadaye mwaka jana kujiunga na Azam FC. Kocha huyo ameweka rekodi ya kuondolewa katika timu mbili alizokuwa akizifundisha ndani ya mwaka mmoja.

Februari mwaka huu alitimuliwa Azam pamoja na Pluijm kwa matokeo ambayo hayakuwaridhisha viongozi na Juni akarejea kuinoa timu yake ya zamani Mbeya City. Hata hivyo alidumu miezi mitano.

Let's block ads! (Why?)

No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...