Search This Blog

Monday, October 11, 2021

KCMC yatoa huduma za bure ikiadhimisha miaka 50

 


Mamia ya wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro wamejitokeza katika viwanja vya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) usharika wa Moshi Mjini, ili kupimwa na kufanya uchunguzi wa magonjwa, zinazotolewa na Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini KCMC.


Huduma hizo zinatolewa ikiwa ni maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa hospitali hiyo yanayotarajiwa kufanyika rasmi Oktoba 16, ambapo wanatoa huduma za vipimo vya uzito, sukari, usikivu, macho, shinikizo la damu, pamoja na magonjwa ya ngozi na zinaa bure.


Wataalamu kutoka hospitali hiyo, pia wanatoa elimu na ushauri wa afya ikiwemo juu ya saratani mbalimbali pamoja elimu na chanjo ya Uviko 19.


Akizungumza leo wakati wa ufunguzi wa wiki ya maadhimisho hayo, katika viwanja vya usharika wa Moshi Mjini, Mkurugenzi Mtendaji wa KCMC Profesa Gileard Masenga, amesema hospitali hiyo imekuwa kimbilio kwa watu wengi katika kanda ya kaskazini na imeweza kupata mafanikio mbalimbali.


Amesema maono ya mwasisi wa hospitali hiyo, Mchungaji Stephano Moshi yalikuwa kujenga hospitali ambayo itatoa tiba ya magonjwa mbalimbali pamoja na kutoa mafunzo kwa wataalamu mbalimbali wa afya na kufanya tafiti za magonjwa ya binadamu, jambo ambalo wanajivunia kulitimiza.


"Tuko hapa leo kutoa shukrani kwa wananchi, kwa kukubali kutuunga mkono na kutembea na sisi kwa kipindi chote cha miaka 50 ambacho tumepita katika hali zote na walitembea na sisi,” amesema.


Aidha, Profesa Masenga ametumia nafasi hiyo kuhimiza wananchi ambao hawajapata chanjo ya uviko 19, kujitokeza kuipata kwa kuwa gharama za kutibu ugonjwa huo ni kubwa na wananchi wengi hawawezi kuzimudu.


"Chanjo ni salama, wengi tumechanja na hatujapata tatizo lolote, chondechonde wananchi jitokezeni kuchanja,” amesema.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mkuu wa Wilaya ya Same Edward Mpogolo ameupongeza uongozi wa hospitali hiyo kwa kuendelea kuenzi maono ya mchungaji Stephano Moshi na kutoa huduma bora.


"Nitoe wito kwa wananchi wa Moshi na Mkoa wa Kilimanjato kwa ujumla, kutumia fursa hii ambayo tumepewa na KCMC kuja kupata huduma hizi za uchunguzi na vipimo bure, maana wakisharudi ndani hatutazipata tena bure," amesema.



No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...