Waziri wa nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu Sera na Bunge, Jenista Mhagama amesema wizara yake inasubiri maelekezo kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan juu ya watendaji waliosababisha baadhi ya miradi ya maendeleo kukataliwa na Mwenge wa Uhuru.
Akizungumza leo oktoba 11, wilayani Chato mkoani Geita ambako mwenge wa Uhuru utazimwa Oktoba 14 mwaka huu, Waziri Mhagama amesema mara zote inapotokea kasoro kwenye miradi wahusika wamekuwa wakichukuliwa hatua na kwamba sasa wanasubiri maelekezo kutoka kwa Rais .
“Ripoti itakayowasilishwa na wakimbiza mwenge wa uhuru kwa utaratibu wa Itifaki ya Mwenge ikiambatana na risala ya utii itakabidhiwa kwa Rais Samia, ambaye kwa uzalendo wake atatoa maelekezo yanayoendana na kile ambacho mwenge umebaini,” amesema Jenista.
Amesema kazi kubwa inayofanywa na mbio za mwenge wa Uhuru ni kuchochea maendeleo kwa kukagua, kufungua na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi ya maendeleo.
Ameitaja pia kazi ya kumulika baadhi ya watendaji ndani ya serikali walioshindwa kutekeleza maagizo na miongozo ya serikali hususan kwenye matumizi sahihi ya rasilimali fedha zinazotafutwa na serikali na kodi za wananchi.
Amesema kila mwaka Mwenge unabeba ujumbe ikiwa pamoja na kutokomeza rushwa, dawa za kulevya kwa vijana, lishe duni kwa watoto na wajawazito, mapambano dhidi ya Ukimwi na kwamba sasa yameongezeka mapambano dhidi ya Uviko 19.
“Mwenge wa Uhuru mwaka huu umehamasisha, kukaguam na kuweka mawe ya msingi, kutembelea na kuzindua miradi 14,145 yenye thamani ya Sh8.3 trilioni nchi nzima.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule amesema maandalizi yote ya kuzima mwenge wa uhuru yamekamilika na kuwataka wananchi kuhudhuria kwa wingi tukio hilo litakalofanyika katika uwanja wa Mazaina wilayani Chato na kuhutubiwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
No comments:
Post a Comment