Search This Blog

Saturday, October 2, 2021

Frelimo kukarabati Chuo cha Kaole Bagamoyo


Na Omary Mngindo, Bagamoyo


CHUO cha Kilimo Kaole kinachomilikiwa na Jumuiya wa Wazazi (CCM) wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani, kinatarajia kuingia makubaliano ya uboreshwaji wa majengo, utayofanywa na Chama Cha Ukombozi cha Frelimo cha Msumbiji.

Makubaliano hayo ni ya ukarabati wa majengo yaliyotumiwa na wapigania Uhuru wa Nchi hiyo yaliyopo chuoni hapo, ambapo mbali ya kuyaboresha majengo husika, pia yatawezesha kuwa sehemu ya Utalii kwa wageni kutokea nchi mbalimbali.

Akizungumza kwenye ziara yake chuoni hapo, Katibu Mkuu wa Frelimo Comrade Roque Salva Samuel alisema kuwa baada ya ombi la uongozi wa Jumuiya hiyo alipotembelea mwaka 2019, sasa Frelimo wamekubali na wameona umuhimu wa kukarabati majengo hayo.

"Chuo cha Kaole ni sehemu muhimu kwa ukombozi wa nchi ya Msumbiji, hivyo kuna historia kubwa inayotakiwa kutunzwa, ili vizazi vitambue uhuru wa nchi yao umechangiwa kwa kiasi kikubwa katika eneo la Bagamoyo nchini Tanzania," alisema Samuel.

Taarifa ya chuo iliyosomwa na Mwalimu Mkuu Simba Simba imeelezea changamoto kadhaa ikiwemo uchakavu wa majengo hayo, hali inayokwamisha kwa namna moja ai nyingine shughuli za kimaendeleo chuoni hapo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuia hiyo Aboubakary Mlawa aliwaambia Waandishi wa habari kuwa, Jumuia inamshukuru Katibu huyo huku akieleza kuwa ukarabati huo utarudisha taswira halisi ya majengo hayo na kuboresha historia halisi ya eneo hilo.

Alisema kuwa nyumba aliyoishi Marehemu Machel, ofisi aliyokuwa anatumia, mabweni ya wapigania uhuru na maeneo yanayoizunguka shule yanahitaji ukarabati mkubwa, ili yaweze kuwa na madhari ya kuvutia zaidi hivyo kuwezesha watu mbalimbali kufika kushuhudia historia hiyo.

"Nchi zingine zilizotumia kituo hiki kilichokuwa cha mafunzo na wapigania uhuru kabla ya kukabidhiwa Jumuiya ya Wazazi mwaka 1975, ni pamoja na Zimbabwe na Afrika kusini," alisema Mlawa.

Aliongeza kuwa Rais Emerson Nnangwaga wa Zimbawe alipotembelea chuoni hapo alitoa fedha kama zawadi kwa chuo wa kutunza kumbukumbu mbalimbali, ambazo walizitumia kwa ukarabati wa baadhi wa mabweni chuoni hapo.

"Umuhimu wa kumbukumbu hizo kukarabatiwa na kutunzwa itakuwa jambo jema, kwani itawapatia fursa vizazi na watu kutoka nchini na mataifa waliyopata Ukombozi wa nchi zao kufahamu historia hiyo, pia kuwa kivutio cha  utali," alimalizia Mlawa.


No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...