
Wauguzi wasio na ajira na wahudumu wa afya kutoka Kenya watapata nafasi ya kufanya kazi nchini Uingereza kama sehemu ya mpango mpya ulioombwa na Serikali ya Kenya na kuzinduliwa na Rais Kenyatta wakati wa ziara yake huko London.
Katika mpango wa kushirikishana maarifa na utaalam, wataalamu wa afya wa Kenya na mameneja wa afya watafaidika na njia maalum ya kufanya kazi nchini Uingereza.
Waziri wa Leba Simon Chelugui alisema serikali imeanza kusafirisha wafanyikazi na wataalamu wenye ujuzi wa hali ya juu nje ya nchi hatua inayolenga kutatua tatizo la uhaba wa wauguzi 62,000 nchini Uingereza.
''Tunasafirisha wauguzi wa Kenya kwenda kufanya kazi nje ya nchi. Mwezi uliopita tulikuwa London na Rais Uhuru Kenyatta na tulifanya mazungumzo na serikali ya Uingereza, ambayo ilikubali kuchukua wahudumu 20,000 kutokana na uhaba wao wa wauguzi 62,000 ambao wamepata mafunzo nchini Kenya,” alisema alipojitokeza kwenye mkutano wa Kamati ya Bunge inayoshughulikia Kazi na Ustawi wa Jamii huko Mombasa.
Makubaliano hayo yako wazi kwa wafanyikazi wa ziada wa afya wa Kenya ambao wana sifa lakini hawana kazi, kuhakikisha mchakato huo unakuwa ni wenye faida kwa Kenya.
Awamu ya kwanza ya wauguzi itaondoka Kenya kufikia Oktoba 15.
No comments:
Post a Comment