Search This Blog

Monday, September 13, 2021

Wafadhili waahidi dola bilioni 1.2 kwa Afghanistan

Mkuu wa misaada ya kiutu wa Umoja wa Mataifa anasema ahadi za dola bilioni 1.2 zimetolewa kwa ajili ya kuwasaidia Waafghani wanaokabiliwa na mzozo wa kiutu unaozidi nchini humo na katika ukanda huo mzima.

Griffiths ameyasema haya mwishoni mwa mkutano wa ngazi ya juu mjini Geneva, uliokuwa unatafuta pia dola milioni 606 hadi mwishoni mwa mwaka kwa ajili ya kuwasaidia watu milioni 11. Mkuu huyo amesema fedha hizo za ziada zimo katika hiyo ahadi ya dola bilioni 1.2.

Griffiths sasa ametoa wito kwa wafadhili kufanya ahadi zao kuwa kweli haraka iwezekanavyo kwa kutoa fedha walizoahidi. Anasema zitawasaidia pakubwa Waafghani hasa wanawake.

"Jukumu la wanawake na wasichana ni muhimu mno kama sehemu yoyote ile. Wanastahili kupata elimu, wanastahili kupata haki zao na huduma zengine muhimu kama ilivyo kwengineko duniani," alisema Griffiths.

Wito wa kuchangishwa fedha kwa ajili ya Afghanistan ulitolewa kutokana na hofu kwamba raia wengi wanakabiliwa na utapia mlo na ukosefu wa chakula nchini humo, huku wengi wengine wakiwa wameyakimbia makaazi yao na kipindi cha majira ya baridi kikiwa kinakaribia.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kutia fedha katika uchumi wa Afghanistan ili kuzuia kuanguka kwa uchumi huo, jambo litakalokuwa na athari kwa raia. Kulingana na Guterres misaada ya kiutu haitotatua matatizo, iwapo uchumi utaanguka ingawa inaweza kutumika kusukuma ajenda ya haki za binadamu nchini humo.

"Iwapo tunataka kulinda haki za binadamu za Waafghani, njia bora ni kuendelea kutoa misaada ya kiutu na kutumia misaada hiyo kuzungumza na Taliban na kusukuma suala la kutekelezwa kwa haki," alisema Guterres.

Naye mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusiana na Haki za Binadamu Michelle Bachelet amesema afisi yake imepokea madai ya kuaminika ya mauaji ya kulipiza kisasi ya maafisa wa zamani wa usalama nchini Afghanistan yanayofanywa na Taliban.

Akizungumza katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa,Bachelet amesema pia maafisa katika serikali iliyopita ya Afghanistan pamoja na familia zao wanakamatwa na kuzuiliwa na baadae wanapatikana wakiwa wamefariki.

Mkuu huyo ametahadharisha kwamba kutakuwa na ukurasa mpya na mbaya kwa Afghanistan kutokana na kukosekana uwiano kati ya maneno ya Taliban na vitendo vyao.

 



No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...