Search This Blog

Friday, September 24, 2021

Serikali kuelimisha wavuvi na kuwapa vifaa vitakavyowasaidia kwenye uvuvi


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imepanga kuwaelimisha  Wavuvi na kuwapa vifaa maalum vitakavyowasaidia kujua wapi kuna makundi ya Samaki ili waachane na Uvuvi wa kuwinda ambao umekuwa hauna tija kwao.


Ulega aliyasema hayo katika hafla fupi ya kuwakabidhi Wavuvi na Wakulima wa Mwani vifaa vya kufanyika kazi vikiwemo injini ya boti na Kamba za kulimia zao la Mwani iliyofanyika katika Kijiji cha  Mchinga, Mkoani Lindi Septemba 23, 2021.


"Sasa hivi tunatumia njia ya 'Satelite' kujua mavuvi yetu yako wapi, samaki wako wapi, kifaa cha GPS kinamsaidia mvuvi kabla hajatoka Pwani kujua  aende umbali gani ambako kuna makundi ya Samaki,"alisema Ulega

Aidha, alitumia nafasi hiyo kuwataka Wavuvi na Wakulima wa zao la Mwani kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuwaletea maendeleo.

Katika hafla hiyo, Naibu Waziri Ulega aliwapatia Wavuvi injini moja ya boti yenye thamani ya Shilingi Milioni 11, na Kamba zenye thamani ya Shilingi Milioni 8 kwa Vikundi vitatu vya kina mama Wakulima wa Mwani Mkoani humo.

Awali, Mbunge wa Jimbo la Mchinga, Mama Salma Kikwete alisema kuwa anaishukuru Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha wananchi wa Jimbo lake vifaa vitakavyowasaidia kufanya shughuli zao kwa ufanisi zaidi.

Aliongeza kuwa yeye kama Mbunge kwa kushirikiana na wananchi ataendelea kuhakikisha maendeleo yanapatiakana kwa kasi katika Jimbo hilo la  Mchinga.



No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...