MKUU wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt. Batilda Buriani amewataka wananchi na Taasisi zote zinazodaiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi na Mazingira Mjini Tabora (TUWASA) kulipa bili zao ili fedha zitakazopatikana zisaidie kuendeleza ujenzi wa miundombinu ya usambazaji maji safi na salama wananchi wengi.
Alisema dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kila mwananchi na anafikiwa na huduma ya majisafi na salama nyumbani kwake na wengine wapata huduma hiyo katika vituo vilivyo karibu na nyumba zao.
Balozi Dkt. Batilda ametoa kauli hiyo leo wakati wa ziara yake ya kikazi ya kutembelea miundombinu ya maji ya TUWASA.
Alisema Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imekusudia ifikapo mwaka 2025 kama ilivyoelekezwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) wananchi wote wanapata huduma ya majisafi na salama majumbani mwao.
Balozi Dkt. Batilda alisema Serikali inaendelea kujenga miundombinu ya maji na kutoa fedha kwa ajili ya shughuli za kumtua ndoo mwanamke na hivyo ni vema kila mtumiaji maji atimize wajibu wake wa kulipia Ankara kila zinapotolewa.
Mkuu huyo wa Mkoa alisema atajitahidi kukutana na Taasisi za Umma zinazodaiwa na TUWASA ili waweze kueleza mpango wa kulipa madeni yao na kuwawezesha kuendeleza kazi nzuri ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wakazi wote kuwa walinzi wa miundombinu ya maji na kuwafichua waharibifu wa mazingira ambavyo ndio vyanzo vya maji.
Alisema tatizo la uchomaji moto mkoani Tabora ni kubwa ni vema Kamati za Mazingira ndani ya vijiji zikatekeleza wajibu wao kwa kuwakamata watu wote wanaochoma moto ovyo na wale wanaolima ndani ya vyanzo vya maji na wanaoendesha shughuli za kibinadamu kinyume cha Sheria.
Kaimu Mkurugenzi Mteandaji wa TUWASA Mayunga Kashilimu alisema baadhi ya wateja wao hasa Taasisi za umma wamekuwa wakitumia huduma ya maji bilia kulipia matumizi yao kwa wakati ambapo hadi hivi sasa wanadaiwa kiasi cha shilingi bilioni 1.
Alisema hali hiyo imesababisha kukwama kwa baadhi ya shughuli za kuongeza miundombinu ya maji safi na salama kwa wateja wao.
Kashilimu alimuomba Mkuu wa Mkoa kuwasaidia kuzikumbusha Taasisi hizo ili fedha hizo iwasaidie katika kuendeleza kazi ya kuboresha miundombinu.
Aidha, alisema Serikali imetenga jumla ya shilingi milioni 600 kwa ajili ya kuanza kuboresha huduma ya maji kwenye Miji ya Sikonge na Urambo.
TUWASA inahudumia wilaya ya Tabora Uyui Sikonge Urambo na Kaliua.

No comments:
Post a Comment