Mahakama Kuu nchini Kenya imeamua kuwa watuhumiwa wote watano- maafisa wanne wa polisi na raia mmoja- wana kesi ya kujibu kuhusiana na mauaji ya Willie Kimani, wakili aliyetekwa nyara na kuuawa Juni, 2016 akiwa na mteja wake Josephat Mwenda na dereva Joseph Muiruri.
Upande wa mashtaka ulifunga kesi yake wiki iliyopita baada ya kuwasilisha mashahidi 46. Upande wa utetezi utaanza kuwasilisha hoja zake wiki ijayo.
Wakili wa utetezi, Cliff Ombeta anasema atawasilisha mashahidi 16. Jaji kisha ataamua ikiwa watano hao wana hatia au la.
Watatu hao walitoweka baada ya Kimani kuwasilisha kesi dhidi ya afisa wa polisikwa niaba ya Mwenda.
Wiki moja baadaye, miili ya watatu hao iliyokuwa imeanza kuoza ilipatikana katika mto, viungani mwa mji mkuu wa Kenya, Nairobi.
Mauaji yao yalizua ghadhabu kali miongoni mwa wanasheria na Wakenya nchini.
Kikosi cha polisi kinatuhumiwa kwa msururu wa mauaji ya kiholela katika miaka ya hivi karibuni

No comments:
Post a Comment