Marekani imetoa wito kwa Rais wa Somalia na Waziri Mkuu kutatua tofauti zao kwa ajili ya ustawi wa nchi.
Ilisema ushirikiano wa viongozi wa Somalia, hususan Rais Mohamed Abdullahi Farmajo na Waziri Mkuu Hussein Roble, ni muhimu kwa nchi "kukamilisha haraka mchakato wake unaoendelea wa uchaguzi".
Mzozo kati ya viongozi hao wawili, uliosababishwa na jinsi serikali ilivyoshughulikia kesi ya jasusi aliyepotea, umezua hofu kwamba mchakato wa uchaguzi wa Somalia unaweza kukumbwa na changamoto nyingi.
Mzozo uliongezeka wiki iliyopita baada ya rais kusimamisha mamlaka ya Utendaji wa Bw Roble, hatua iliyotajwa na waziri mkuu kuwa "haramu".
''Tunatoa wito kwa Rais na Waziri Mkuu waepuke matamko au vitendo vya uchochezi na kusuluhisha kutokubaliana kwao juu ya uteuzi wa wafanyikazi na mamlaka zao kwa amani,” taarifa ya msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje Ned Price ilisema.
Taifa hilo la Pembe la Afrika limepangwa kufanya uchaguzi wa bunge moja kwa moja kati ya 1 Oktoba na 25 Novemba.
Marekani inasema kuwa kuchelewesha zaidi kwa uchaguzi kunaweza kuongeza "uwezekano wa vurugu na kutoa nafasi kwa al-Shabab na vikundi vingine vyenye msimamo mkali kusambaratisha nchi".

No comments:
Post a Comment