Na Tegemeo Kastus.
Utaratibu wa usambazaji wa maji wa kanda utendelea kama kawaida badala ya wazo la viongozi
wa kijiji cha malekchand kutaka utaratibu wa umwagiliaji ufanyike kwa kijiji. Maelekezo hayo
yamemaliza mvutano uliokuwepo katika ukanda wa mfereji wa maji (scheme) unaosambaza
katika vijiji viwili vya Laghangarer na Malekchand. Maamuzi hayo yanalenga kutoharibu
maamuzi yaliyofikiwa awali kati ya jumuiya ya watumia maji bonde la kati singida , viongozi wa
skimu kutoka vijiji vyote vinavyozunguka bonde la Eyasi, wataalamu na wadau wanaojihusisha
na kilimo cha umwagiliaji tarafa ya Eyasi.
Hayo yamejiri katika mikutano ya hadhara ambayo Mkuu wa wilaya ya Karatu Mh. Abbas
Kayanda alipokuwa akizungumza na wananchi wa vijiji vya Laghangarer na Malekchand.
Amesema utaratibu wa umwagiliaji wa kanda lazima ufuatwe, ameongeza kusema wataalamu wa
maji kutoka bonde la kati Singida wamepima maji katika mifereji inayosambaza maji katika
kijiji cha Laghangarer na Malekchand. Na kwa mujibu wa vipimo hivyo walibaini kasi ya maji
katika mifereji inayosambaza maji Laghangarer ni Lita 432 kwa sekunde na kasi ya mifereji
inayosambaza maji kwa kijiji cha Malekchand ni lita 414 kwa sekunde.
Mh. Kayanda ameelekeza Juwamaboe pamoja na wataalamu wa maji bonde la kati Singida,
kufanya upembuzi yakinifu wa gharama za kuweka mlango katikati ya kiungo cha kusambazia
maji kwenye mfereji wa vijiji vya Laghangarer na Malekchand. Amesema baada ya gharama
kufahamika Juwamaboe waandike barua kwa viongozi wa vijiji kuwajulisha gharama za ujenzi
huo ili maji yaweze kugawanya kwa usawa na kuondoa tofauti wa lita 18 za maji
zinazolalamikiwa katika mgao wa maji kwa kanda baina ya vijiji hivyo.
Mh. Kayanda amesema mabadiliko ya tabia ya nchi na kuongeza kwa shughuli za kibinadamu
yanaendelea kusababisha maji kupungua. Amesema Halmashauri imetenga fedha kwa ajili ya
kumalizia ujenzi wa visima viwili vilivyochimbwa katika kijiji cha Malekchand. Amesema
mwaka wa fedha 2022-2023 Halmashauri ya wilaya itatenga fedha kwa ajili ya kuchimba visima
vya maji katika kijiji cha Laghangarer. Amesema kulingana na kasi ya ufunguaji wa mashamba
ya kilimo inavyoendelea ni vyema sasa wakulima wakajiunga kwenye vikundi ili kuanza
kuchimba visima vyao ili kukabiliana na upungufu wa maji kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji
katika bonde la Eyasi. Kama walivyo fanya wakulima wanaojihusisha na kilimo cha umwagiliaji
wa vitunguu na mahindi katika eneo la Midabini na kitongoji cha Kambi ya simba.
Wakati huo huo Mh. Kayanda amewapongeza wananchi wa vijiji vya Laghangarer na
Malekchand kwa jitihada za kuanza ujenzi wa sekondari ya Eyasi ili kupunguza adhaa ya
wanafunzi kutembea umbali mrefu. Amehimiza wananchi kuendelea kujitoa kwa ajili ya ujenzi
wa shule ya sekondari ya Eyasi. Amesema ili shule ya sekondari ya Eyasi iweze kuanza lazima
ujenzi wa maabara, ujenzi wa ofisi ya walimu ujenzi wa madarasa ukamilike. kabla ya wakaguzi
wa elimu wa kanda kukagua ili kutoa kibali kwa shule kuanza kupokea wanafunzi.
Mh. Kayanda ameelekeza kamati ya ujenzi wa shule hiyo kusimamisha ujenzi wa nyumba ya
mwalimu mpaka mwahandisi atakapowapatia ramani ya ujenzi ya serikali. Ameelekeza
Mwandisi wa wilaya kufanya ushauri wa kitaalamu ikiwa ni pamoja na kufanya setting ya
msingi kabla ujenzi wa nyumba hiyo kuanza. Katika hatua nyingine Mh. Kayanda amewaelekeza
viongozi wa serikali za vijiji vya Laghangarer na Malekchand kuweka mipaka ya eneo la shule
ya sekondari Eyasi ili eneo hilo lisije likavamiwa.
Katika hatua nyingine Mh. Kayanda amehimiza viongozi wa Halmashauri ya kijiji kujua mipaka
ya kazi zao za uongozi, amesema ni vyema Mwenyekiti akajua majukumu yake kama kiongozi
wa kisiasa wa kijiji na Afisa mtendaji kijiji akajua majukumu yake kama Mtendaji wa shughuli
zote zinazofanyika kwenye kijiji. Amesema wajumbe wa kijiji wanapaswa pia kujua wajibu wao
katika kushauri serikali ya kijiji, na kusimamia shughuli za mendeleo katika vitongoji vyao.
Amesema viongozi wakifanya kazi kwa ushirikiano hakutakuwa na mvutano au malumbano
katika kusimamia miradi ya maendeleo. Amesema mivutano ya uongozi ndio inayosababisha
wananchi kukosa ari ya kujitoa kwenye shughuli za maendeleo.






No comments:
Post a Comment