Jeshi la Polisi mkoani Mara na uongozi wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha), wameendelea kurushiana mpira kuhusu madai ya kukamatwa kwa viongozi watatu wa baraza hilo. Pia, kongamano la kudai Katiba Mpya lililopangwa kufanywa na Bavicha limeshindwa kuanza kwa wakati kutokana na sintofahamu hiyo.
Wakati Bavicha ikidai kukamatwa kwa makada wao watatu jana usiku, Polisi kwa upande wake imekana madai hayo ikisema kuwa, hakuna kada wa chama hicho anayeshikiliwa.
Lakini, Bavicha limesisitiza kuwa Polisi walivamia ofisi zao jana usiku na kuwakamata baadhi ya makada wakati wakiendelea na maandalizi kwa ajili ya kongamano hilo lililopangwa kuanza leo Jumamosi Septemba 4, 2021.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi Septemba 4, 2021 Kaimu Katibu Mkuu wa Bavicha Taifa, Yohana Kahunya amesema makada haoa ambao hawajafahamika majina mara moja walipewa jukumu la kupanga viti, kuandaa mahema na maandalizi mengine ya mkutano huo walikamatwa saa sita usiku wa kuamkia leo Jumamosi wakati wakiendelea na majukumu hayo katika viwanja vya ofisi ya Chadema eneo la Nyakato kwa Saanane mjini Musoma.
"Bado sijapata majina yao lakini polisi walifika na kuruka ukuta kisha kuingia ndani na kuwakamata watu hao na hawakuishia hapo tu walichukua na 'matenti' (mahema) pamoja na viti zaidi ya 200 vilivyopangwa kwa ajili ya kongamano hilo na mpaka sasa bado wapo polisi," amesema Kahunya.
Kuhusu kuchelewa kuanza kwa kongamano hilo, Kuhanya amesema ameshangazwa na kitendo kilichofanyika na Polisi na vyombo vingine vya usalama kuzingira ofisi za chama hicho kwa madai ya kufanya usafi.
"Sisi wenyewe imebidi tutumie mbinu mbadala kupita pale kwa sababu tusingeweza kupita tukiwa tumevaa sare na hakuna namna unavyoweza kuingia ofisini kwani, polisi wamejaa getini kwa madai kuwa wanafanya usafi. Tunafahamu lengo ni kuhakikisha wanazuia kongamano lisifanyike," amesema na kuongeza kuwa: “Kongamano hilo litafanyika licha ya vikwazo hivyo vya polisi na kwamba, sasa litafanyika kuanzia saa 7:00 mchana badala ya asubuhi kama ilivyopangwa”.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi mkoa wa Mara, Longinus Tibishibwamu licha ya kukanusha vijana wake kuwashikilia watu hao, pia amesema hawataruhusu kufanyika kwa kongamano hilo kwa kuwa ni ni kinyume cha sheria.
"Rais alishatoa maelekezo kuwa sasa hivi watu wajielekeze kwenye ujenzi wa uchumi na kama unavyojua tupo kwenye uchumi wa kati hivyo, Serikali inalenga kuboresha uchumi twende kwenye uchumi mkubwa zaidi kwa hiyo hayo makongamano yasubiri wakati mwingine,"amesema Kamanda Tibishibwamu alipozungumza na Mwananchi kwa njia ya simu.
Pia, amesema madai ya Polisi kuzingira ofisi za Chadema hayana ukweli kwa kuwa, wananchi na taasisi zingine zikiwemo za ulinzi na usalama ziko kwenye kampeni ya kufanya usafi hivyo, wapo eneo hilo kwa ajili ya kufanya usafi na sio kudhibiti Chadema.

No comments:
Post a Comment